************************
PARIS, UFARANSA.
Wafadhili wa Afya ya Mama na Mtoto -Global Financing Facility For Women, Children and Adolescent (GFF) kuipatia Tanzania msaada wa dola milioni 25 sawa na shilingi za Kitanzania bilioni 57 kwa ajili ya kuboresha huduma za afya ya mama na mtoto nchini.
Hayo yamebainishwa leo kwenye Mkutano wa 14 wa GFF ambapo Tanzania inawakilishwa na Waziri wa Afya Ummy Mwalimu jijini Paris,Ufaransa.
Waziri Ummy amesema kuwa Wizara ya Afya imejipanga kuelekeza angalau asilimia 80 ya fedha hizo kwenye Zahanati , vituo vya afya na hospitali za Halmashauti ili kuboresha huduma.
Waziri Ummy amekiambia kikao hicho kuwa Tanzania imepiga hatua katika utoaji wa hufuma za mama na mtoto na zipo dalili ya kupungua kwa vifo vitokanavyo na uzazi na watoto.
“Tanzania ina historia ndefu ya huduma za afya za msingi,Serikali zote zilizopita hususani Mhe.Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Awamu ya nne ya Jamhuri ya Tanzania aliweka mkazo mkubwa kwenye huduma za afya ya msingi”.Alisema.
Hata hivyo Waziri Ummy amesema kuwa bado Tanzania ina kazi kubwa ya kufanya ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya na kwa wakati hivyo amewaomba wafadhili hao kuendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania.
“Tunawaomba tuendelee kushirikiana ili kuboresha huduma za afya ya mama na mtoto katika kipindi hiki ambacho Tanzania inajivunia kuwa na Rais wa kwanza Mwanamke Mhe. Samia Suluhu Hassan.
Mkutano wa 14 wa wafadhili wa Afya ya Mama na Mtoto unafanyika jijini hapa kuanzia tarehe 6 hadi 8 Juni, 2022 ni mkutano muhimu wa wadau katika ustawi wa Sekta ya Afya na unajadili masuala mbalimbali ikiwemo uimarishwaji wa huduma za afya katika ngazi ya msingi.
Vilevile kikao hiki kinajadili changamoto zilizopo na mafanikio yaliyopatikana kupitia ufadhili wa GFF pamoja na namna bora ya kuongeza rasilimali watu kwenye vituo vya kutolea huduma za afya ikiwemo kuwapatia mafunzo mahususi watumishi wa afya na kuwaongezea vitendea kazi ili kuboresha huduma zinazotolewa kwenye vituo vya afya ngazi ya msingi.