- Majadiliano yafanyika pembezoni mwa Mkutano Mkuu wa Maendeleo ya Mawasiliano Duniani – ITU WTDC – 2022 Kigali, Rwanda
Na Mwandishi Maalum/ Kigali, Rwanda
Tanzania inatarajia kunufaika kwa ushiriki wake kwenye Mkutano Mkuu wa Maendeleo ya Mawasiliano Duniani (ITU WTDC – 2022), unaofanyika jijini Kigali – Rwanda, kujadili na kuweka mipango ya Maendeleo katika Sekta ya Mawasiliano Duniani; ukiandaliwa na Shirika la Mawasiliano la Umoja wa Mataifa (ITU). Mkutano huo unafanyika kwa mara ya kwanza barani Afrika ukilenga kuweka mikakati ya kuhakikisha jamii zote duniani zinaunganishwa kwenye mifumo ya mawasiliano.
Katika Mkutano huo Tanzania ilikutana na kufanya mazungumzo na Serikali ya Australia kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Biashara ya nchi hiyo, ambapo mbali na kuomba uungwaji mkono ili nchi hiyo iipigie kura Tanzania kuwa mjumbe wa Baraza la ITU pia walijadili masuala ya kuongeza ushirikiano kwenye maeneo ya sera, masuala ya ufundi na taluma na utafiti.
Akizungumzia mazungumzo hayo yaliyofanyika pembezoni mwa ITU WTDC – 2022 Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Dkt. Jabiri Bakari alibainisha kuwa Australia imekubali kuiunga mkono Tanzania katika maeneo yote ya majadiliano na kwamba imefurahishwa na ushiriki wa taasisi za elimu ya juu kwenye mkutano huo wa Rwanda.
“Kiufupi tumekubaliana kushirikiana na Australia kwenye maeneo matatu, eneo la sera, eneo la taaluma na utafiti, masuala ya kiufundi kwenye eneo lote la TEHAMA ambayo yanahusisha usalama mtandaoni, wameonesha kuvutiwa kwao na uwepo wa vyuo vikuu vitatu UDOM UDSM na DIT na kuahidi kuendeleza mashirikiano kati yao na taasisi za elimu ya Juu za Tanzania” alibainisha Bakari.
ITU kupitia idara yake ya Maendeleo ya Mawasiliano (BDT), huandaa Kongamano la Dunia la Maendeleo ya Mawasiliano (WTDC) kila baada ya miaka minne ili kupokea mada mbalimbali, kujadili utekelezaji na uanzishwaji wa miradi na programu muhimu kwa maendeleo ya mawasiliano ulimwenguni na kuangazia ukuaji wa sekta ya mawasiliano duniani. Aidha, ITU WTDC – 2022 ni chombo cha juu zaidi cha kutunga sera cha ITU ambacho pia kupitisha mipango ya kimkakati na kifedha ya miaka minne, na kuchagua timu ya wasimamizi wakuu wa shirika, nchi wanachama wa Baraza, na wanachama wa Bodi mbalimbali za Shirika hilo lililopo chini ya Umoja wa Mataifa (UN).
Ikiwa ni mwanachama hai na mshiriki wa mkutano huo, Tanzania itatumia fursa hiyo kuomba uungwaji mkono kutoka nchi wanachama wa ITU kuchaguliwa kuwa mjumbe wa Baraza la ITU kwenye mkutano mkuu wa Shirika hilo utakaofanyika mjini Bucharest, Romania, itakapowadia mwezi Septemba baadae mwaka huu.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Dkt. Jabiri Bakari akizungumzia vipaumbele vya mdhibiti wa huduma za mawasiliano nchini Tanzania alisisitiza kuwa Mamlaka anayoiongoza imejidhatiti kuwa mshiriki anaekwenda sambamba na mabadiliko ya teknolojia kwa kuhakikisha inashirikiana na nchi nyingine duniani kupokea na kuyatekeleza mageuzi muhimu ya TEHAMA.
“Matarajio yetu ni kuona mkutano huu unaiwezesha TCRA kuelewa upi hasa ni mwelekeo wa sekta ya mawasiliano na TEHAMA katika ujumla wake duniani ili nasi kama nchi tusiachwe nyuma; ushiriki wetu unaipa Mamlaka nguvu ya kuwa mshiriki thabiti kwenye mabadiliko mbalimbali ya kiteknolojia duniani; hasa ukizingatia kuwa sekta ya mawasiliano ina kasi kubwa ya ukuaji, nasi tunataka kuwa sehemu ya mabadiliko hayo,” alifafanua Bakari na kuongeza.Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Dkt. Jabiri Bakari akifuatilia mada kwenye Mkutano Mkuu wa Maendeleo ya Mawasiliano Duniani (ITU WTDC – 2022), unaofanyika jijini Kigali – Rwanda. Picha Na: TCRA.
Kwenye mkutano huo wa Septemba, Tanzania itaomba kuchaguliwa kuwa miongoni mwa nchi wanachama wa Baraza la ITU, ikizingatiwa kuwa imekuwa kitovu cha kuziunganisha nchi zilizo mbali na ufuo wa bahari ya Hindi kwenye mkongo wa mawasiliano upitao baharini; hivyo ujumbe kwenye Baraza hilo utamaanisha kutetea maslahi ya ukanda wa Afrika hasa Kusini mwa Jangwa la Sahara katika masuala ta ukuzaji TEHAMA. Hadi sasa Tanzania inaziunganisha nchi za Uganda, Rwanda, Burundi, Msumbiji, Malawi, na Kenya na mkakati ni kuendelea kusambaza huduma za Mkongo wa Mawasiliano katika nchi nyingi zaidi ikiwemo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Akizungumzia dhima ya ushiriki wa Tanzania Meneja wa Sehemu ya Usimamizi wa Rasilimali za Mawasiliano na Teknolojia wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania Mhandisi Mwesiga Felician alibainisha kuwa Tanzania inashiriki katika kutoa maazimio mbalimbali ya sekta ya Mawasiliano duniani huku ikitarajia kutumia fursa ya uwepo wa mkutano huo kuomba uungwaji mkono na kupigiwa kura kuwa Mjumbe wa Baraza la Utendaji la Shirika la Mawasiliano Duniani (ITU) kwenye mkutano mkuu wa ITU unaotarajiwa kufanyika nchini Romania mwezi Agosti baadae mwaka huu.
“Tanzania imekuwa nchi yenye ushawishi wa TEHAMA kwenye ukanda wetu, lengo letu ni kuhakikisha tunatumia fursa ya mkutano huu kujinadi ili tuingie kwa mara nyingine kuwa mjumbe wa Baraza la ITU wakati wa Mkutano Mkuu hapo mwezi Septemba mwaka huu kwani hii ni fursa ya kuongeza ushawishi wetu katika kukuza TEHAMA katika ukanda huu wa Afrika” alibainisha Felician na kuongeza kuwa, ushiriki wa Tanzania kama mjumbe wa Baraza la ITU utaiwezesha nchi Kusimamia masuala muhimu katika kukuza uchumi wa Kidijitali.
ITU husimamia sekta tatu yaani sekta ya viwango, sekta ya maendeleo ya TEHAMA, na sekta ya masafa. ITU WTDC – 2022 ulitanguliwa na Kongamano la Mtandao wa Vijana lililofanyika Juni 2-4 mwaka huu jijini Kigali, kujadili masuala mtambuka ya sekta mbalimbali za uchumi na namna TEHAMA inavyoweza kuchangia ukuaji wa uchumi kupitia sekta hizo kwa kadri TEHAMA inavyorahisisha ukuaji huo; na Tanzania ilishiriki kikamilifu kupitia uwakilishi wa Mamlaka ya Mawasiliano na ujumbe wa Vijana waliojikita katika fani za TEHAMA kutoka taasisi za elimu ya juu.
Ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano huo unaongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Jim Yonaz akisaidiwa na Mkurugenzi wa Masuala ya Kisekta Dkt. Emmanuel Mannaseh anaeongoza ujumbe wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania, Mamlaka ya Mawasiliano inayoshiriki kama msimamizi mkuu wa sekta ya mawasiliano nchini Tanzania. Wawakilishi wengine ni kutoka taasisi za elimu ya juu ambazo ni Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) na Chuo Kikuu cha St. Joseph cha jijini Dar es salaam.
Picha ya pamoja ya Ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano Mkuu wa Maendeleo ya Mawasiliano Duniani (ITU WTDC-2022), unaofanyika jijini Kigali, Rwanda; ukiongozwa na Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Jim Yonazi, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Dkt. Jabiri Bakari na washiriki kutoka Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania. Mkutano huu ulioanza Juni 6,2022 utahitimishwa Juni 16, 2022.
***********************