Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Dkt. Isaac Maduhu akizungumza wakati wa Ufunguzi wa Mafunzo ya ‘Graphic Designing’ kwa Maafisa Habari, Mawasiliano na Uhusiano wa Wizara na Vyombo vya Usalama vilivyopo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, yaliyofanyika katika Ukumbi wa Mikitano ofisi ya Wizara, Mtumba, jijini Dodoma
Naibu Katibu Mkuu,Dkt.Isaac Maduhu akikabidhi vyeti vya kutambua ushiriki wa Vitengo vya Habari na Mawasiliano vilivyopo Wizarani na vya Vyombo vya Usalama vya Wizara hii katika kutangaza Mafanikio ya Wizara na Taasisi zake katika kipindi cha Miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndanj ya Nchi Dkt. Isaac Maduhu akiwa kwenye picha ya pamoja na Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,Christina Mwangosi, Wasemaji wa Vyombo vya Usalama vilivyopo Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi pamoja na Maafisa Habari, Mawasiliano na Uhusiano wa Wizara hii.
………………………………………….
Na Mwandishi wetu,
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi imesema inatambua mchango mkubwa unaotolewa na Vitengo vya Habari, Mawasiliano na Uhusiano vya Vyombo vyote vya Usalama vilivyoko chini ya Wizara hiyo katika suala zima utoaji wa taarifa na elimu kwa Umma kuhusu masuala mbalimbali yanayotekelezwa na Jeshi la Polisi, Magereza, Zimamoto na Uokoaji, Idara ya Uhamiaji na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA).
Hayo yamesemwa leo na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Dkt. Isaac Maduhu Kazi alipokuwa akifungua mafunzo ya siku kumi ya “graphic designing” kwa Maafisa Habari, Mawasiliano na Uhusiano wa Wizara, na Vyombo vyote vya Usalama vilivyopo katika Wizara hiyo.
Dkt. Maduhu amesema kuwa kupitia Vitengo vya Habari, Mawasiliano na Uhusiano vilivyopo kwenye Vyombo vya Usalama vilivyopo Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, elimu na taarifa kwa umma zimekuwa zikitolewa na hivyo kuifanya jamii kufahamu masuala mbalimbali yanayohusu Wizara na Vyombo vyake pamoja na mafanikio mbalimbali yanayopatikana.
Amesema kuwa kutokana na mabadiliko ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano yanayoenda kwa kasi Wizara imeona ni vema kuandaa mafunzo ya “graphic designing” kwani kwa sasa ni ujuzi unaohitajika sana kwenye Vitengo vya Habari, Mawasiliano na Uhusiano ili kufikisha taarifa, na elimu kwa Umma kupitia mfumo huo wa utoaji wa taarifa, na kwamba hivi sasa jamii inahitaji habari iliyo katika mfumo huo wa “infographic” zaidi.
“Mafunzo haya ya siku kumi yatawasaidia watendaji katika Vitengo hivyo kupata ujuzi ambao utasaidia kuboresha utendaji kazi wa Vitengo hivyo, hali itakayosaidia kupunguza utegemezi wa wataalamu wa nje na kuongeza ufanisi katika kutekeleza majukumu ya Wizara na Vyombo vyake vya Usalama.” Alisisitiza.
Amesema sambamba na Wizara kuandaa mafunzo hayo muhimu, Wizara pia imevikabidhi Vitengo vya Habari, Mawasiliano na Uhusiano vya Vyombo hivyo vya Usalama Vyeti vya aina mbili vya kutambua ushiriki wa kila Kitengo katika kutangaza Mafanikio ya Wizara na Taasisi zake katika kipindi cha miaka 60 ya uhuru wa Tanzania Bara na kutangaza Mafanikio ya Wizara na Taasisi zake katika kipindi cha Mwaka Mmoja wa Serikali ya Awamu ya Sita.
Naibu Katibu Mkuu Dkt. Maduhu amewasisitiza Wasemaji wa Vyombo hivyo na Maafisa Habari, Mawasiliano na Uhusiano kuendeleza ushirikiano katika utekelezaji wa majukumu kwa kuwa jambo hilo litaongeza tija na ufanisi katika kutekeleza majukumu ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.