Meneja wa Mradi kutoka Misa Tanzania Bi.Neema Kasubiro akifafanua jambo kwa washiriki
Mtayarishaji vpindi Edward Lucas kutoka kituo cha redio Mazingira akielezea mafanikio na changamoto katika uandaaji wa vpindi vya usawa wa kijinsia katika kituo hicho.
Mtayarishaji vpindi Glory Kusaga kutoka kituo cha redio Uvinza akielezea mafanikio na changamoto katika uandaaji wa vpindi vya usawa wa kijinsia katika kituo hicho.
TAASISI ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika tawi la Tanzania (MISA TANZANIA) imeendelea juhudi zake za kuwanoa waandishi wa habari ili kukuza usawa wa kijinsia kupitia vipindi vya radio za kijamii nchini.
MISA TANZANIA kwa kushirikiana na Vikes inaendesha mradi wa kuwajengea uwezo waandishi kutoka katika radio za kijamii nchini ili kutengeneza vipindi vitakavyoleta mabadiliko katika usawa wa kijinsia ikiwemo uhuru wa kujieleza miongozi mwa wanawake.
Akizungumza baada ya kikao kazi cha kupata mrejesho kutoka kwa waandishi kutoka mikoa mbalimbali nchini kilichofanyika jijini Dodoma mwishoni mwa wiki,Meneja mradi huo Neema Kasubiro amesema katika kipindi cha utekelezaji wa mradi huo kuna mabadiliko yanayoonekana katika uandaaji wa vipindi vya usawa wa kijinsia.
“Baada ya kuwajengea uwezo waandishi wa habari, wapo waliofikia hatua ya kuanzisha vipindi katika radio zao hili waweze kufanyia kazi elimu wanayoipata kuhusu usawa wa jinsia katika maudhui ya vipindi vya radio zao” alifafanua.
Neema amesema mradi huo utekelezaji wake umegawanyika katika awamu mbalimbali na kwa awamu hii ilianza January na itakamilka mwaka 2024 ikitarajiwa kujikita Zaidi katika kuboresha ubora wa maudhui katika mada za jinsia.
Akizungumza baada ya kusikiliza vipindi mbalimbali vilivyoandaliwa na waandishi hao,mwandishi mkongwe nchini Abubakar Famau amesema kwamba ili sauti za wanawake zisikike katika vyombo vya habari ni lazima waandishi wawe tayari kushirikisha jamii katika uandaaji wa vipindi vyao.
“Kama tutawashirikisha kwa kiwango kinachotakiwa nina uhakika lengo la kupata uhuru wa kujieleza kutoka kwa kundi kubwa la wanawake litatimia” alisema Famau.
Pia Famau amewataka waandishi na watangazaji wa vipindi vya redio nchini kufuata misingi ya uzalishaji wa vipindi hivyo ikiwemo matumizi sahihi ya lugha ya Kiswahili ili waweze kufikisha ujumbe kwa wasikilizaji kama ilivyokusudiwa.
Famau amebainisha kwamba bado kuna matatizo katika matamshi na uchaguzi usio faa wa maneno kwa baadhi ya watangazaji wa redio nchini.
Hata hivyo kwa upande wa waandishi wa habari washiriki wa mradi huo wamebainisha kuwa licha ya mafanikio yaliyopatikana tangu kuanza kwa utekelezaji wa mradi huo bado kuna changamoto zinazohitajika kutatuliwa ili kutimiza malengo.
Mratibu wa vipindi kutoka kituo cha radio cha Mazingira kilichopo wilayani Bunda,mkoani Mara Lucas Edward amesema ufinyu wa waandishi wa habari wa kujikita katika habari za jinsia imekuwa changamoto kubwa katika utekelezaji.
Kwa upande wake Glory Kusaga,mtangazaji wa kituo cha radio cha Uvinza toka mkoani Kigoma amesema uwepo wa mfumo dume katika jamii bado unaathiri ushiriki wa wanawake katika maudhui ya redio hivyo kuwa kikwazo kwa watayarishaji.
“Tunahitaji sana sauti za jinsia zote zisikike katika vipindi vyetu,lakini bado kuna wanawake hawawezi kuongea kwenye redio hadi wapate ruhusa za waume zao”amesema akiongeza kuwa hali hiyo husababisha wanawake kushindwa kushiriki kikamilifu kutoa maoni yao katika vyombo vya habari.
5.