Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu ameitaka Bodi ya Taasisi ya Taifa ya utafiti wa magonjwa ya Binadamu (NIMR)
kuharakisha mchakato wa kuanza kutoa chanjo dhidi ya ugonjwa wa Malaria kwa wananchi.
Waziri Ummy amesema hayo leo katika uzinduzi wa Baraza jipya la Taasisi hiyo uliofanyika leo hii Jijini Dar es salaam.
Waziri Ummy amesema NIMR imeshiriki kufanya utafiti wa kupata chanjo ya malaria ambayo tayari imesha thibitishwa na shirika la afya Duniani kuwa inafaa kutumika.
“Kwahiyo naomba mfanye mchakato haraka wa kuanza kutoa chanjo, kwa kuanzia chanjo hiyo itatolewa kwa yule ambae yupo tayari kulipia kwa gharama zitakazo wekwa lakini Serikali itaangalia kama itaweza kutoa kwa watoto chini ya miaka mitano”. Amesema Waziri Ummy.
Aidha, Waziri Ummy ameitaka NIMR kuweka nguvu katika kuhakikisha wanafanya tafiti zenye kuleta manufaa kwa wananchi ili kuiwezesha Serikali kuchukua maamuzi haraka katika utoaji wa huduma za Afya Nchini.
“Zaidi ya asilimia 60 ya Watanzania wanatumia dawa za tiba asili lakini watu wanakunywa dawa bila kufuata dozi maalum, sasa naitaka NIMR itupe ushahidi wa kisayansi juu ya dawa hizo na dozi inayo hitajika kwa dawa husika”. Ameongeza Waziri.
Nae Mganga mkuu wa Serikali Dkt. Aifello Sichalwe amelitaka Baraza hilo kuwa kiunganishi kizuri kati ya sekta ya Afya na watafiti mbalimbali wa masuala ya Afya wa ndani na nje ya nchi.
“Natumaini Bodi itasaidia kuweka mazingira bora katika kuifahamisha Wizara kwa ajili ya maamuzi na utungaji wa sera lengo ni kuharakisha mchakato wa kupata vibali bila kuathiri thamani na ubora wa tafiti”. Amesema Dkt. Sichalwe
Kwa upande wake Mwenyekiti wa bodi hiyo Dkt. Andrew Kitua wakati wa kutoa shukurani ameahidi kushirikiana na wizara pamoja na taasisi zingine za utafiti ili kufanya tafiti zenye kuleta manufaa kwa wananchi.