Katibu Mkuu wa JOWUTA, Selemani Msuya akizungumza katika mkutano wa Chama hicho ambacho walikaa na waandishi wa habari kueleza ni namna gani wamejipanga na kupata wanachama wapya.Mkutano huo umefanyika Juni 03, 2022 Jijini Dar es Salaam Katibu Mkuu wa JOWUTA, Selemani Msuya akisisitiza jambo katika mkutano wa Chama hicho ambacho walikaa na waandishi wa habari kueleza ni namna gani wamejipanga na kupata wanachama wapya.Mkutano huo umefanyika Juni 03, 2022 Jijini Dar es Salaam Mwanachama wa Chama Cha Wafanyakazi wa Vyombo vya Habari Tanzania (JOWUTA) Bw.Lisungu Kambona akizungumza katika mkutano wa Chama hicho ambacho walikaa na waandishi wa habari kueleza ni namna gani wamejipanga na kupata wanachama wapya.Mkutano huo umefanyika Juni 03, 2022 Jijini Dar es Salaam Baadhi ya wanachama wa Chama Cha Wafanyakazi wa Vyombo vya Habari Tanzania (JOWUTA wakifuatilia mkutano wa Chama hicho ambacho walikaa na waandishi wa habari kueleza ni namna gani wamejipanga na kupata wanachama wapya.Mkutano huo umefanyika Juni 03, 2022 Jijini Dar es Salaam.
(PICHA ZOTE NA EMMANUEL MBATILO)
****************************
Na Mwandishi Wetu
WAANDISHI wa Habari nchini wameshauriwa kujiunga na Chama Cha Wafanyakazi wa Vyombo vya Habari Tanzania (JOWUTA), ili waweze kushirikiana kudai haki zao kwa pamoja.
Ushauri huo umetolewa na Katibu Mkuu wa JOWUTA, Selemani Msuya leo wakati akiwaelezea waandishi wa Mkoa wa Dar es Salaam faida za kujiunga na chama hicho.
Msuya alisema JOWUTA ni chama chenye umuhimu kwao hivyo wanapaswa kukitumia kwa mujibu wa sheria.
Alisema JOWUTA imeamua kuiwaita na kuwaeleza umuhimu wa wao kujiunga na chama hicho ambacho ndicho kina mamlaka kisheria ya kudai, kutetea na kusimamia haki na maslahi ya waandishi wa habari nchini.
“Kwa mujibu wa Sheria Ajira na Mahusiano Kazini ya Mwaka 2004, nyie kama waandishi wa habari mna haki ya kujiunga na JOWUTA, ili tuweze kushirikiana pamoja kudai na kutetea haki zetu, hakuna mtu atatoka taasisi nyingine kudai haki zetu.
Nawaomba mjiunge JOWUTA kwani ndio sehemu sahihi kwa tasnia hii katika kudai haki zetu hizo taasisi nyingine kwa mujibu wa Sheria haziwezi kufanya hivyo,”alisema Msuya.
Katibu huyo alisema Serikali ipo tayari kufanya kazi na JOWUTA, hivyo kinachohitajika ni wao kujiunga ili kuwa na nguvu kubwa ya pamoja.
Msuya alisema madhila wanayopitia waandishi wa habari nchini hasa kukosa mikataba ya ajira inatokana na wao kutokuwa kitu kimoja.
Katibu huyo alisema asilimia 70 ya waandishi wa habari nchini hawana mikataba pamoja na kuwa na sifa za kitaaluma jambo ambalo halikubaliki kwa mujibu wa sheria.
Katibu huyo alisema JOWUTA inataka waandishi kuungana ili kuondokana na watu wanaoitwa correspondent au retainer ambao kwenye taaluma zingine hawapo.
“Umoja ni nguvu, utengano ni udhaifu, niwaombe ndugu zangu njooni JOWUTA tuunganishe nguvu, ili kuweza kudai haki zetu kwa pamoja. Nasisitiza kuwa hakuna mtu atakaa mbele kudai haki zetu tofauti na sisi wenyewe,” alisema.
Aidha, Msuya alisema kutokana na waandishi wengi kukosa mikataba hawachangii kwenye mifuko ya hifadhi ya jamji, hawana bima na stahiki nyingine kama mafao kwa mujibu wa sheria.
Msuya aliwataka waandishi hao kuwa mabalozi kwa mabosi wao ili waweze kuwapa ushirikiano wa kuunda vyama vya wafanyakazi katika maofisi yao.
Alisema JOWUTA kwa mujibu wa Katiba yake inapokea wafanyakazi wote wanaofanya kazi kwenye vyombo vya habari.