Msururu wa magari zaidi ya 50 yaliyokuwa yamewabeba vijana wa UVCCM ukielekea kwenye Hifadhi ya Ngorongoro kwa ajili ya kutembelea vivutio vya utalii.Lengo ya UVCCM kuandaa safari hiyo ni katika kuunga mkono kwa vitendo jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan kuutangaza Utalii wa Tanzania kupitia Filamu ya The Royal Tour.
*****************
Na Mwandishi Wetu, Ngorongoro
UJUMBE wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) zaidi ya 1,000 wakiongozwa na Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo Taifa Kenani Kihongosi umewasili katika Hifadhi ya Ngorongoro kwa lengo la kufanya utalii wa kutembelea vivutio mbalimbali vilivyopo ndani Hifadhi hiyo.
Akizungumza leo Juni 4,2022 , Katibu Mkuu wa UVCCM Taifa Kenan Kihongosi ameeleza lengo la ziara hiyo ni kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kwenye fimalu ya The Royal Tour ambayo imeonyesha vivutio mbalimbali vilivyopo ndani ya Nchi yetu.
“Vijana hawa zaidi ya 1,000 wamekodisha magari ya utalii 140 na wameamua kujigharamia kuja hapa Ngorongoro kuona vivutio tulivyonavyo ili kusaidia kutoa hamasa na chachu kwa watanzania wengine wajue kuwa Utalii unaanza na sisi wenyewe ili tuwe mabalozi wa kuhamasisha wageni wengine wa nje ya Nchi kukutembelea” alifafanua Kihongozi
Ameongeza uwepo wao katika maeneo ya Wilaya za Karatu na Ngorongoro umesaidia kuongeza mzunguko kwa wajasiriamali hasa Hoteli, Magari ya utalii, biashara za vyakula kwa mama lishe hivyo kusaidia uimarishaji uchumi wa wananchi katika kusukuma agenda ya maendeleo na kuwaambia watu kuwa utalii ni fursa na utalii ni ajira.
Akipokea Ujumbe huo Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro Raymond Mwangala amewashukuru UVCCM kwa kuunga mkono jitihada za Rais na Serikali yake kuhamasisha utalii wa ndani kwa vitendo kwa kuamua kuchangishana kwa kwa idadi kubwa kutembelea vivutio vya Ngorongoro kwa pamoja.
Ameeleza kuwa Vivutio vya Ngorongoro ni vya kipekee na baada ya uzinduzi wa Filamu ya Royal tour anaamini wageni wataongezeka na kuongeza mapato ya Serikali ambayo yataongeza uchumi wa Nchi na kusaidia Serikali katika ujenzi na uimarishaji wa huduma zingine za kijamii kwa wananchi wake.
Kwa upande wake Kamishna Msaidizi Mwandamizi Elibariki Bajuta anayesimamia huduma za Ulinzi NCAA ameuhakikishia ujumbe huo kuwa eneo la Hifadhi ya Ngorongoro ni Salama, tulivu lenye vivutio vya Kila aina na Serikali kupitia NCAA inaendelea na juhudi za Uhifadhi na uboreshaji wa miundimbinu ya Utalii ili wageni wanaotembelea Hifadhi hiyo kupata huduma bora muda wote.