Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma Mhe. Abdi Kagomba akufunga mafunzo kwa watumishi na wadau (hawapo pichani) wa kituo Jumuishi cha Utoaji Haki jijini Dodoma yaliyolenga uboreshaji wa utoaji huduma kwa mteja katika Ukumbi wa mikutano wa IJC yaliyofanyika kwa muda wa siku tano
Msajili wa Mkuu wa Mahakama ya Tanzania akitoa mada ya huduma kwa mteja wakati wa mafunzo kwa watumishi na wadau wa kituo Jumuishi cha Utoaji Haki jijini Dodoma, mafunzo yakilenga uboreshaji wa utoaji huduma kwa mteja katika Ukumbi wa mikutano wa IJC.
Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma Bw. Sumera Manoti akichangia Mada wakati wa mafunzo hayo.
Sehemu ya watumishi na wadau wa Kituo Jumishi cha Utoaji Haki Jijini Dododma wakifuatilia mada ya huduma ya kwanza wawapo kazini aliyesimama mbele ni mwezeshaji wa mafunzo hayo.
Sehemu ya watumishi na wadau wa Kituo Jumishi cha Utoaji Haki Jijini Dododma wakifuatilia mafunzo hayo (wa kwanza hadi wa nne meza ya kushoto ni Majaji wa kituo hicho).
(Picha na Innocent Kansha – Mahakama)
………………………………
Na Innocent Kansha – Mahakama, Dodoma.
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma Mhe. Abdi Kagomba amewaasa watumishi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki jijini Dodoma kutumia mafunzo waliyoyapata ili yatumike kama silaha ya kuongeza kasi ya uwajibikaji na kuepuka kufanya kazi kwa mazoea ikiwa ili kupunguza urasimu usio wa lazima katika kutoa huduma kwa wananchi na watumishi.
Akizungumza katika hafla ya kufunga mafunzo hayo yaliyotolewa kwa watumishi na wadau wa kituo chicho katika Ukumbi wa mikutano yaliyofanyika kwa muda wa siku tano ambayo yaliyolenga uboreshaji wa utoaji huduma kwa mteja, leo tarehe 3 June, 2022 Jaji Kagomba alisema, Malengo ya kuanzishwa vituo hivi jumuishi yatadhihiri kwa watanzania kushuhudia mabadiliko ya utoaji huduma kwa mwananchi.
“Hivyo ni wajibu wetu kuyafanyia kazi tuliojifunza ili kutatua changamoto tunazokutana nazo na kuongeza ufanisi wa utekelezaji wa majukumu yetu. Tutumie mafunzo haya kuwa waadilifu na kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zinazoongoza Utumishi wetu, kwa kuwatendea wengine vile ambavyo tungependa sisi kutendewa”, alisema Jaji Kagomba.
Hata hivyo, Jaji Kagomba alisistiza kuwa, malalamiko na maoni ya wananchi yashughulikiwe kwa ufanisi na weledi, kwa wakati katika ngazi zote. Alisema ni dhahiri ubora wa mafunzo yaliyotolewa yatawaondolea wananchi na wateja adha ya kutopata huduma bora ambazo zinatolewa na kutatuliwa kituoni hapo.
“Mambo kama uadilifu na weledi, ikiwa ni pamoja na kutumia vipawa mlivyokirimiwa vitasaidia kubuni njia sahihi za kutatua changamoto zinazowakabili kaika utoaji wa huduma bora, bidii katika kazi, ushirikiano kama timu na nidhamu ya dhati katika utekelezaji wa kazi ikiongozwa na uzalendo, uchamungu ndiyo msingi mkuu katika utendaji”, alisisitiza Jaji Kagomba.
“Mhe Kagomba aliongeza, naomba niwasisitizie kuendelea kujikumbusha namna ya kutekeleza mambo yote niliyoyataja hapo juu, kila mara, mtakapokuwa mkitekeleza majukumu yenu ya kila siku. Na pia, mtatakiwa kuendelea kuhuisha aina za huduma zinazotolewa na Taasisi kila panapotokea mabadiliko ili kuuwezesha utoaji bora wa huduma na haki”,.
Akielezea mada zilizofundishwa Jaji Kagomba alisema kuwa, anafahamu kuwa katika siku zote za mafunzo yaliyofundishwa na kukumbushwa ni maeneo muhimu ambayo watumishi wamekuwa wakikutana nayo katika utekelezaji wa majukumu kwa wadau wa Mahakama, kama vile, umuhimu wa kulinda Maadili ya Utumishi wa Umma, Tunu na utamaduni sahihi wa Mahakama, namna ya kushughulikia malalamiko na kero za wapokea huduma zetu, uboreshaji wa utoaji Huduma kwa wateja, kuongeza ufanisi na weledi katika kazi na namna ya kutoa huduma ya kwanza.
Mhe. Kagomba, aliendelea kueleza kuwa, mafunzo yaliyotolewa ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Mahakama wa 2021/22 hadi 2024/2025 unaotafsiri kwa vitendo maono ya uongozi wa juu wa nchi yetu, na pia ya Kiongozi Mkuu wa Muhimili wa Mahakama, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma katika kuhakikisha usimamizi na utoaji wa huduma katika utumishi wa Umma unaendelea kuwa wa haki na wenye kufuata misingi ya uwazi, uadilifu, uwajibikaji na weledi, bila kusahau uzalendo, na yakifanya hayo yote kwa kumjali mteja ambaye ni mwananchi anayehudumiwa.
Mafunzo hayo yalizinduliwa rasmi katika Kituo hicho, jijini Dodoma, siku ya Jumatatu, tarehe 30 Mei, 2022 na yalilenga kujengea uwezo watumishi na wadau namna bora ya kushughulikia utoaji wa huduma za kimahakama, kubadilishana uzoefu katika kushughulikia malalamiko na kupokea maoni ikiwa ni pamoja na kubaini changamoto zinazojitokeza katika kushughulikia malalamiko na namna ya kukabiliana na changamoto hizo.