Na mwandishi wetu, Simanjiro
Mwenyekiti wa ECLAT Foundation, Peter Toima ameikabidhi Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro, Mkoani Manyara, madarasa tisa, ofisi mbili za walimu, madawati 89, matenki mawili ya mfumo wa kuvunia maji, vyoo viwili vyenye matundu 32 ya shule ya msingi Nadonjukini Kata ya Komolo..
Toima akizungumza wakati wa makabidhiano ya miundombinu hiyo iliyogharimu shilingi milioni 290 amesema ECLAT Foundation wameshirikiana na Upendo Society katika kufanikisha kazi hiyo.
Amesema baada ya kuombwa kusaidia ujenzi wa madarasa ya shule hiyo ya Nadonjukini hakusita kwani aliona changamoto iliyopo na kuanza kuifanyia kazi mara moja.
Mkuu wa wilaya ya Simanjiro Dk Suleiman Serera amempongeza Toima kwa kukabidhi madarasa hayo ambayo yatachochea upatikanaji wa elimu kwa wanafunzi wa jamii ya wafugaji wa eneo hilo.
“Leo asubuhi nilikuwa Dodoma, nikapitia Babati kisha nikaja Nadonjukini kutokana na umuhimu wa tukio hili la maendeleo ya wanafunzi wetu,” amesema Dk Serera.
Mbunge wa Jimbo la Simanjiro, Christopher Ole Sendeka amemshukuru Toima kwa kufanikisha ujenzi wa madarasa tisa ya shule hiyo na kuwataka wadau wengine wa maendeleo wafike Simanjiro.
“Mwalimu Toima ni mdau wa maendeleo hivyo wadau wengine waje Simanjiro wafanye maendeleo bila kuwa na tatizo lolote kwani maendeleo ndiyo suala la kwanza,” amesema Ole Sendeka.
Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Simanjiro, Baraka Kanunga amewashukuru ECLAT Foundation na Upendo Society kwa kufanikisha ujenzi huo.
“Tunawashukuru mno kwa maendeleo haya kwani hata diwani mstaafu wa Komolo Michael Haiyo amekuja kushiriki tukio hili,” amesema Kanunga.
Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Nadonjukini, Thabitha Namfua amesema shule hiyo ilianzishwa mwaka 2000 ikiwa na wanafunzi 30 na sasa ina wanafunzi 680.
Mwalimu Namfua amesema anamshukuru mkazi wa Nadonjukini, Noah Mombashi (Simbaa) kwa kujitolea kuwapa maji kwa ajili ya ujenzi wa madarasa matatu mapya na ofisi.