*****************
Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria Bi. Mary Makondo ameagiza wananchi wote wenye watoto wa umri chini ya miaka mitano kuwasajili na huduma hiyo inatolewa bure.
Bi. Makondo ametoa agizo hilo wakati akizindua Mpango wa usajili wa watoto wa umri chini ya miaka mitano katika mkoa wa Tabora, leo tarehe 03 Juni, 2022, ambapo hadi sasa Mikoa 22 nchini imenufaika na mpango huo tangu ulipozinduliwa hapa nchini mwaka 2015.
Mpango huo unatekelezwa na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) kwa kushirikiana na Wadau mbalimbali wa Maendeleo una lengo la kuboresha hali ya usajili wa vizazi nchini.
Mbali na kufungua mlango wa haki ya kutambuliwa kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano, mpango huo umekuwa na matokeo makubwa ya utatuzi wa changamoto mbalimbali zilizokuwa zinaikabili Serikali na wananchi kuhusiana na usajili wa vizazi.
“Cheti cha kuzaliwa ni haki ya kila mtoto aliyezaliwa katika ardhi ya Tanzania awe raia na asiye raia, kinachotakiwa ni wazazi wa mtoto husika kuthibitisha uraia wao kabla taratibu za kumsajili mtoto hazijaanza,” alisema Bi. Makondo.
Aidha, amewataka wananchi kutoa msaada na ushirikiano katika zoezi la utambuzi wa wazazi wenye sifa za kusajili watoto wao ili wapewe vyeti vya kuzaliwa.
Serikali imeipongeza RITA, Ofisi za Wakuu wa Mikoa na Wilaya pamoja na Mamlaka za Serikali za Mitaa katika Mikoa yote ambayo Mpango huu unatekelezwa kwa namna wanavyoratibu zoezi hili kwa ufanisi mkubwa.
Kwa kutambua mchango mkubwa wa Wadau wa Maendeleo katika utekelezaji wa mpango huo, Bi. Makondo ameshukuru Shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia Watoto (UNICEF) na Serikali ya Canada.
Aidha, ameshukuru Kampuni ya Mawasiliano ya TIGO pamoja na wadau wengine kwa kuendelea kuwa sehemu ya utekelezaji wa mpango huu muhimu kwa maendeleo ya nchi yetu.
Kwa upande wa Watendaji wa Kata na Wasajili katika Vituo vya Afya, Bi. Makondo amewaagiza kufanya kazi kwa weledi, uadilifu na uzalendo wa hali ya juu. “Serikali haitamfumbia macho yeyote atakayekiuka taratibu na kukwamisha Mpango huo,” alisema.
Kwa pamoja wadau wa maendeleo kutoka UNICEF na Canada wamesema wataendelea kuunga mkono juhudi za Serikali kuhakikisha hakuna mtoto atakayeachwa bila kusajaliwa.