Afisa Usalama wa Chakula Mwandamizi TBS, Bi. Immaculata Justin akizungumza na waandishi wa habari leo katika Makao Makuu ya Shirika la Viwango Tanzani (TBS) Jijini Dar es Salaam.Afisa Usalama wa Chakula TBS, Bi. Mary Lihuluku akizungumza na waandishi wa habari leo katika Makao Makuu ya Shirika la Viwango Tanzani (TBS) Jijini Dar es Salaam.
************
NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
KATIKA kuelekea Siku ya Usalama wa Chakula Duniani, Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limewataka wananchi kila mmoja achukue nafasi yake katika kuhakikisha chakula kinakuwa salama kwa mlaji ili kuepuka magonjwa yanayosababishwa na kula chakula kisichokuwa salama.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Juni 3,2022 katika Ofisi za TBS Jijini Dar es salaam, Afisa Usalama wa Chakula Mwandamizi TBS, Bi. Immaculata Justin amesema katika kuadhimisha siku ya usalama wa chakula duniani TBS imelenga kuinua uelewa wa jamii kuhusiana na usalama wa chakula na umuhimu wake katika sekta ya afya pamoja na uchumi.
” Chakula kisipokuwa salama kinaweza kusababisha magonjwa lakini pia hata uchumi utashuka kwasababu unapotibiwa fedha zitatumika na biashara ya chakula ndani na nje ya nchi inaathirika kwasababu chakula kisicho salama kinaweza kusababisha kumwagwa au kukataliwa katika soko, hii ni hasara kwahiyo uchumi wa nchi unashuka”. Amesema
Amesema maadhimisho haya yamekuja kwa lengo la kuhamasisha jamii yetu kuhakikisha kwamba inazalisha chakula ambacho ni salama lakini pia wale ambao wanahusika na usafirishaji, uhifadhi au uandaaji wa chakula chenyewe kwa maana hiyo mnyororo mzima wa chakula kuanzia shambani au mjini kuhakikisha kwamba chakula kinakuwa salama mpaka kinapomfikia mlaji.
Aidha amesema kuwa kwenye maadhimisho hayo wanajiunga na nchi zingine Duniani itakapofikia tarehe ya maadhimisho hayo ambayo hufanyika Juni 7 kila mwaka ikizingatiwa kwamba madhara yatokanao na chakula kisichokuwa salama yanaathiri jamii lakini pia yanaathiri uchumi.
Ameeleza kuwa Takwimu zilizotolewa na Shirika la Afya Duniani ziinaonesha kwamba takribani watu Milioni 6 huugua kila mwaka kwasababu ya kula chakula kisichokuwa salama lakini pia kuugua huku kunasababisha vifo ambapo takribani watu laki 420 hufariki.
Kwa upande wake Afisa Usalama wa Chakula TBS, Bi. Mary Lihuluku amesema kuwa inabidi wadau wote kuweka nguvu katika kuhakikisha kwamba chakula ni salama , kwamba ni jukumu la kila mtu kuhakikisha chakula kinakuwa salama kwa mlaji..