**************************
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), ni Idara huru ya Serikali inayojitegemea, ambayo imeundwa kupitia Ibara ya 129(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977. Ibara ya 130(1), (c), (f) na (g) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977 na vifungu vya 6(1) (c) na (g), 15(1) (a) na 28(1) (a), (b) na (f) vya Sheria ya THBUB Sura 391, vimeipa THBUB mamlaka ya kuchunguza jambo lolote linaloashiria au kuthibitisha uvunjaji wa haki za binadamu au ukiukwaji wa misingi ya utawala bora nchini. Vilevile, kifungu cha 6(h) kinaipa THBUB mamlaka ya kutembelea magereza na sehemu wanapozuiliwa watu kwa lengo la kukagua uzingatiaji wa haki za binadamu katika sehemu hizo.
Jukumu la msingi la Jeshi la Polisi ni kulinda usalama wa raia na mali zao, pamoja na majukumu mengine yaliyoainishwa katika Sheria za Jeshi la Polisi ikiwemo kukamata, kufanya upekuzi, kuwaweka watuhumiwa mahabusu, kufanya upelelezi kuhusiana na matukio ya uhalifu na kufanya mahojiano na watuhumiwa. Sheria ya Jeshi la Polisi na Huduma Saidizi, Sura ya 322, Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai Sura ya 20 na Kanuni za Jeshi la Polisi za Mwaka 2013, zimeainisha mamlaka hayo ya Polisi na utaratibu unaopaswa kufuatwa wakati wa utekelezaji wa mamlaka hiyo.
Tathmini ya ujumla ya THBUB inaonesha kuwa Jeshi la Polisi linafanya kazi zake vizuri na ndio maana kwa sasa kuna amani na utulivu nchini na uhalifu umepungua. Hata hivyo, pamoja na tathmini hiyo ya ujumla, kwa nyakati tofauti kumekuwa na malalamiko kutoka kwa watuhumiwa na wananchi na wakati mwingine kupitia vyombo vya habari kulalamikia Jeshi la Polisi kuhusu matukio ya uvunjwaji wa haki za binadamu na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora.
Kuanzia mwaka 2020 hadi 2022, THBUB imekuwa ikifuatilia mwenendo na utendaji kazi wa Jeshi la Polisi kwa kufanya chunguzi kumi (10) zinazohusu tuhuma dhidi ya Jeshi hilo pamoja na kutembelea vituo vya polisi katika baadhi ya mikoa nchini. THBUB pia imekuwa ikiwatembelea mahabusu waliozuiliwa katika magereza ambako pia ilipata taarifa za malalamiko ya mahabusu kuhusu kuvunjiwa haki zao walipokuwa katika mahabusu za polisi. Chunguzi hizo zilifanyika katika Wilaya ya Kinondoni, Ubungo na Ilala katika Mkoa wa Dar es Salaam; Wilaya ya Mwanga katika Mkoa wa Kilimanjaro; Wilaya ya Kilosa na Mvomero katika Mkoa wa Morogoro; na Wilaya ya Tabora mjini kwa Mkoa wa Tabora. Pia THBUB ilifanya chunguzi katika Wilaya ya Mafinga kwa Mkoa wa Iringa; Wilaya ya Handeni kwa Mkoa wa Tanga; Wilaya ya Masasi kwa Mkoa wa Mtwara; na Mkoa wa Mjini Magharibi, Zanzibar.
Katika kipindi hicho THBUB pia ilitembelea baadhi ya vituo vya Polisi kwa lengo la kukagua uzingatiaji wa haki za binadamu katika vituo hivyo. Vituo vilivyotembelewa ni kutoka Mkoa wa Dar es Salaam, Pwani, Tanga, Dodoma, Mwanza, Ruvuma, Lindi na Mtwara. Mikoa mingine ni Mjini Magharibi, Kaskazini Unguja, Kusini Unguja, Kaskazini Pemba na Kusini Pemba.
Katika chunguzi na ziara hizo, THBUB ilibaini mambo yafuatayo:
- i) Kupigwa na kuteswa kwa watuhumiwa wakati wa ukamataji, au wakati upelelezi ukiendelea kwa madhumuni ya Jeshi la Polisi kupata taarifa zinazohusu matukio ya uhalifu ikiwemo watuhumiwa kupata madhara ya mwili na wakati mwingine kupoteza maisha;
- Kuwepo tuhuma za rushwa dhidi ya baadhi ya askari;
- Baadhi ya Askari Polisi kutoa taarifa zisizo sahihi kuhusu vitendo wanavyolalamikiwa na wananchi;
- Askari Polisi wanaopatikana na hatia kupewa adhabu isiyowiana na kosa husika;
- Baadhi ya watuhumiwa kuwekwa mahabusu za Polisi kwa muda mrefu bila ya kupelekwa mahakamani au kupewa dhamana; na
- Uhaba wa vitendea kazi, uchache wa nyumba za kuishi askari, uchache wa Askari Polisi na miundombinu chakavu katika vituo vya Polisi.