Meneja wa NEMC Kanda ya kaskazini ,Lewis Nzali akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha leo.(Happy Lazaro)
***********************
Happy Lazaro, Arusha.
Arusha.Halmashauri zimetakiwa kushirikiana na wadau mbalimbali pamoja na makampuni binafsi katika kuhakikisha wanafikia malengo yaliyowekwa ya kupanda miti 1.5 milioni kwa mwaka.
Hayo yamesemwa leo jijini Arusha na Meneja wa NEMC Kanda ya kaskazini ,Lewis Nzali wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake katika kuelekea siku ya mazingira duniani Juni 3,2022 itakayofanyika mkoani Dodoma.
Lewis amesema kuwa, katika kuhakikisha mazingira yanalindwa na kutunzwa katika maeneo mbalimbali ,halmashauri zote zimewekewa malengo ya kuhakikisha wanapanda miti 1.5 milioni kwa mwaka ,japo halmashauri nyingi hazijaweza kufikia lengo kutokana na changamoto mbalimbali ikiwemo rasilimali fedha.
Amesema kuwa, halmashauri zinatakiwa kushirikiana na wadau , makampuni na Taasisi binafsi ili waweze kufikia malengo hayo huku wakizitumia pia Taasisi za fedha na kwa kufanya hivyo wataweza kufikia malengo hayo na kuweza kuwafikia watu wengi zaidi.
“Ni vizuri pia halmashauri wakazitumia shule vizuri na kupita kwenye shule mbalimbali huku wakijipanga katika kuhakikisha wanazitumia hizo kwa kupeleka miti ya kutosha huku lengo likiwa ni kufikia malengo waliyojiwekea ya kila mwaka.”amesema.
Amesema kuwa, kauli mbiu ya siku ya mazingira duniani kitaifa ni “Tanzania ni moja tu,tunza mazingira huku kauli mbiu ya kimataifa ikiwa ni”Dunia ni moja tu ,tunza mazingira”huku kimataifa ikiadhimishwa nchini Sweden .
Lewis amefafanua,katika kuelekea siku ya mazingira NEMC kanda ya kaskazini akishirikiana na wadau mbalimbali wameweza kuweka alama za mipaka kandokando ya mto Naura ulioratibiwa na Bonde la Mto Pangani ambapo alama za mipaka zimewekwa katika umbali wa mita 60 kutoka katika chanzo cha maji kwa kuzingatia sheria ikiwemo sheria ya usimamizi wa Mazingira.
Amefafanua kuwa, katika shughuli ya uwekaji wa alama za mipaka (Beacons) 70 ziliweza kuwekwa kandokando ya Mto Naura ,sambamba na upandaji wa miti katika kata ya Mkonoo ambapo jumla ya miti 250 ilipandwa katika shule za msingi na sekondari Mkonoo.
Lewis amesema kuwa, Baraza litaendelea kushiriki katika shughuli mbalimbali ambazo zimepangwa kwa kushirikiana na wadau wake ikiwemo usafi wa Mazingira katika maeneo mbalimbali,kushuhudia maonesho ya wadau kuhusu teknolojia,ubunifu,na mbinu za uhifadhi na usimamizi wa Mazingira katika wilaya ya Arumeru na kuendelea kutoa elimu kuhusu hifadhi na usimamizi wa Mazingira.