Meneja wa Ruwasa wilaya ya Songea Mhandisi Mathias Charles kushoto, akitoa taarifa ya ujenzi wa mradi wa maji Magagura wilaya ya Songea kwa Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge
Tenki la kuhifadhia maji linaloendelea kujengwa katika mradi wa maji Magagura wilayani Songea kupitia fedha za Mpango wa maendeleo kwa ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya Uvico-19.
Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge kulia, akimsikiliza meneja wa Ruwasa wilaya ya Songea Mathias Charles wakati alipotembelea mradi wa maji Magagura unaotekelezwa na kwa fedha za mpango wa maendeleo kwa ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya Uvico-19.
Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge kulia,akimsikiliza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya Songea Neema Maghembe wakati mkuu huyo wa mkoa alipofanya ziara ya siku moja katika Halmashauri hiyo kukagua na kutembelea miradi wa maji inayotekelezwa na Ruwasa.
……………………………
Na Muhidin Amri,Songea
MKUU wa mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge,ametoa muda wa mwezi mmoja kuanzia jana kwa kampuni ya Jambela Ltd inayojenga mradi wa maji katika kijiji cha Magagura Halmashauri ya Songea vijijini,kukamilisha ujenzi wa mradi huo haraka ili uweze kuwaondolea wananchi kero ya kutembea umbali mrefu kufuata huduma ya maji kwa matumizi yao ya kila siku.
Brigedia Jenerali Ibuge,ametoa agizo hilo jana baada ya kutembelea mradi huo akiwa katika ziara yake ya siku mbili kukagua ujenzi wa miradi ya maji inayotekelezwa na Serikali kupitia fedha za mpango wa maendeleo kwa ustawi wa Taifa na mapambano dhidi ya Covid-19.
Alisema,fedha zilizotengwa kutumika katika mradi wa maji Magagura ni nyingi, kwa hiyo lazima Mkandarasi ahakikishe anajenga mradi huo kwa viwango ili uendane na thamani halisi ya fedha zilizotolewa na Serikali kama ilivyo kwenye makubaliano ya mkataba.
Brigedia Jenerali Ibuge,ameuagiza uongozi wa Wakala wa usambazaji maji safi na usafi wa mazingira vijijni(Ruwasa)wilaya ya Songea kusimamia kwa karibu mradi huo na wahakikishe unajengwa kwa viwango ili uweze kudumu kwa muda mrefu.
“muda mliompa wa siku kumi na tano na asilimia za utekelezaji wa kazi zilizofanyika hata ukiniambia anaweza kumaliza kazi zilizobaki sikubaliani na wewe hata kidogo, tafadhali sana naomba fedha zilizotolewa na serikali zisichezewe hata kidogo,nataka mradi huu ukamilike haraka kama mlivyokubaliana katika mkataba na sio vinginevyo”alisema Brigedia Jenerali Ibuge.
Awali Kaimu Meneja wa Ruwasa wilaya ya Songea Mhandisi Mathias Charles alisema kuwa,ujenzi wa mradi wa maji Magagura ulipangwa kuhudumia kijiji kimoja tu cha Magagura chenye watu takribani 3,675 na unatekelezwa na Mkandarasi kampuni ya Jambela Ltd ya Songea.
Alisema,mkataba wa ujenzi wa mradi huo ni miezi minne na ulianza kutekelezwa tarehe 14 Januari 2022 na ulitakiwa uwe umekamilika tarehe 21 Mei lakini waliongeza muda wa utekelezaji hadi tarehe 15 Juni 2022 kutokana na changamoto zilizojitokeza wakati wa utekelezaji wake.
Alimueleza Mkuu wa mkoa kuwa,fedha zilizopangwa kutekeleza mradi huo ni Sh.milioni 512,655,273.90 ambapo gharama ya mkandarasi ni Sh.326,751,681.90 kupeleka umeme Sh.27,797,850.00,kununu na kufunga pampu za kusukuma maji Sh.28,500,000.00.
Alisema Sh.129,605,742.00 zimetumika kama gharama ya bomba na hadi sasa Sh.332,954,470.80 sawa na asilimia 65 ya gharama ya mradi zimeshalipwa kutokana na kazi zilizofanyika.
Alitaja kazi zilizopangwa kutekelezwa ni kujenga tenki la kuhifadhia maji lenye ujazo wa lita 150,000,ununuzi wa bomba,ujenzi wa nyumba za mitambo,kujenga vituo 16 vya kuchotea maji,kufunga mfumo wa umeme.
Aidha alisema kazi nyingine zilizopangwa kutekelezwa katika mradi huo ni kununua pampu,kuchimba mtaro,kulaza na kuunganisha bomba pamoja na kufikiwa mitaro umbali wa km 16.1 na kuunganisha maji kwenye vituo vyote 16.
Alisema kuwa, katika utekelezaji wa mradi changamoto kubwa ilikuwa ni kasi ndogo ya hasa nyakati za mvua,hata hivyo mkandarasi chini ya usimamizi wa Ruwasa atafanya kazi usiku na mchana ili mradi huo ukamilike kwa muda uliopangwa.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Kampuni ya Jambela Ltd Valentine Kapinga alisema,kuchelewa kwa mradi huo kumetokana na changamoto ya mvua kubwa zilizonyesha kwa wingi na kusababisha kushindwa kufikisha vifaa kwenye mradi kwa wakati.
Hata hivyo, amehadi kufanya kazi usiku na mchana na amemshukuru Mkuu wa mkoa Brigedia Jenerali Ibuge kwa kuwaongezea muda wa mwezi mmoja ambao watautumia kukamilisha kazi hiyo.