Mkurugenzi wa bodi ya maji bonde la mto Pangani,Segule Segule akizungumza katika hafla hiyo Jijini Arusha (Happy Lazaro)
Meya wa jiji la Arusha,Maximilian Iraqhe akiweka udongo katika Beacon kwenye chanzo Cha maji (Happy Lazaro)
************************
Happy Lazaro ,Arusha.
Arusha.Meya wa jiji la Arusha,Maxmilian Iraghe amewataka maofisa mipango miji kujithimini katika utendaji kazi wao kwa kuhakikisha wanadhibiti makazi holela katika vyanzo vya maji katika maeneo mbalimbali jijini Arusha.
Aidha maofisa hao wametakiwa kujitathmini juu ya utoaji vibali vya ujenzi katika maeneo ya hifadhi ya vyanzo vya maji ndani ya mita 60.
Meya ameyasema hayo jijini Arusha wakati wa uzinduzi wa kampeni ya uwekaji wa mipaka(Beacons) katika hifadhi ya vyanzo vya maji jijini Arusha,ambapo amesema kuwa, anawashangaa maafisa mipango miji kutoa vibali vya ujenzi katika hifadhi ya mito hivyo ni vyema wakachukua tahadhari mapema.
“Kupitia hilo napenda kutoa rai kwa wananchi wa jiji la Arusha kuhakikisha wanatunza mazingira katika vyanzo vya maji na kuendesha shughuli za kibinadamu pembezoni mwa mito ndani ya mita 60 ni kinyume na sheria,”amesema Meya.
Amesema kuwa, kupitia zoezi hilo la uwekaji wa alama ni kuwajulisha ujenzi walioufanya ndani ya mita 60 sio mahali sahihi na mito inayoongoza kwa makazi ya watu ni mto Ngarenaro,Kijenge na Themi hivyo ni vyema wadau wa mazingira wakawekeza elimu katika maeneo hayo.
Hata hivyo amesema kuwa,pamoja na bonde la Pangani kuweka alama hizo kwa ajili ya kuwajulisha wananchi maeneo ya hifadhi ya mito ambayo hairuhusiwi pia halmashauri ya jiji la Arusha wataongeza beaconi kwa ajili ya kumalizia zoezi hilo.
Mkurugenzi wa bodi ya maji bonde la mto Pangani,Segule Segule amesema ili kuhakikisha vyanzo vya maji vinakuwa endelevu ni lazima kuanzia katika vyanzo husika na kusimamia kwa lengo la kuhakikisha hayaleti madhara kwa watu.
“Maji pia yasipotumika vyema yanaweza kuwa ni silaha mbaya kwa binadamu na kutokana na vyanzo hivho kuwepo katika sehemu mbalimbali ushiriki wa wadau ni muhimu sana ni vyema kila mmoja akatekeleza wajibu wake katika nafasi yake katika maeneo mbalimbali,”amesema.
Segule Segule amesema zoezi hilo la uwekaji alama limeanza katika mto Naura lengo ni pamoja na kuhamasisha utunzaji wa vyanzo vya maji ikiwa shughuli za binadamu zinatakiwa kufanyika nje ya mita 60 kingo za vyanzo.
Kwa upande wake Afisa mazingira kutoka bodi ya maji bonde la mto Pangani,Felista Joseph amesema changamoto zilizopo katika mto Naura ni pamoja na shughuli za kibinadamu,ujenzi wa makazi ya watu katika eneo la chanzo cha mto Naura na utupaji wa taka ngumu.
Ameongeza kuwa ,shughuli mbalimbali za binadamu zimekuwa zikiathiri ubora wa maji hivyo uwekaji wa alama hizo zitakwenda kuondoa baadhi ya changamoto hizo ili anapokiuka sheria atapata adhabu kwa mujibu wa kanuni.
Mwisho.