Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye (kulia), akizungumza wakati wa kikao cha kukabidhiwa ripoti ya tathimini ya hali ya mawasiliano pamoja na hatua mbalimbali zilizochukuliwa na Kampuni ya Simu ya Vodacom kufuatia malalamiko ya watumiaji wa huduma za mawasiliano alipokutana na viongozi wa mtandao huo leo Juni 1, jijini Dodoma.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Simu ya Vodacom, Sitholizwe Mdlalose akifafanua jambo wakati wa kikao cha kukabidhi ripoti ya tathimini ya hali ya mawasiliano pamoja na hatua zilizochukuliwa na Kampuni hiyo kufuatia malalamiko mbalimbali ya watumiaji wa huduma za mawasiliano kilichofanyika leo Juni 1, jijini Dodoma. Kikao hicho kilihudhuriwa na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye.
Mkurugenzi anayeshughulikia Maswala ya Kisekta kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Nchini (TCRA), Dk Emmanuel Manase akizungumza wakati wa kikao cha kukabidhi ripoti ya hali ya mawasiliano ya mtandao wa Vodacom nchini kilichofanyika leo Juni 1, jijini Dodoma. Kikao hicho pia kilihudhuriwa na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye pamoja na viongozi wa Vodacom nchini.
Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uhusiano wa Vodacom, Rosalynn Mworia akifafanua jambo wakati wa kikao cha kukabidhi ripoti ya tathimini ya hali ya mawasiliano pamoja na hatua zilizochukuliwa na Kampuni hiyo kufuatia malalamiko mbalimbali ya watumiaji wa huduma za mawasiliano kilichofanyika leo Juni 1, jijini Dodoma. Kikao hicho kilihudhuriwa na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye.
Viongozi wa Vodacom Tanzania wakifatilia maelekezo ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye (hayupo pichani) wakati wa kikao cha kukabidhiwa ripoti ya tathmini ya hali ya mawasiliano pamoja na hatua mbalimbali zilizochukuliwa kufuatia malalamiko ya watumiaji wa huduma za mtandao huo nchini leo Juni 1, jijini Dodoma.
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye (kulia), akizungumza jambo na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Simu ya Vodacom, Sitholizwe Mdlalose (katikati) pamoja na Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uhusiano wa Vodacom, Rosalynn Mworia mara baada ya kikao cha kukabidhiwa ripoti ya tathmini ya hali ya mawasiliano pamoja na hatua mbalimbali zilizochukuliwa kufuatia malalamiko ya watumiaji wa huduma za mtandao huo nchini leo Juni 1, jijini Dodoma.
………………………………………….
Na Alex Sonna-DODOMA
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye, ameiagiza Mamlaka ya Mawasiliano nchini (TCRA) pamoja na Kampuni za simu kukomesha tabia ya kuunganisha wateja kwenye huduma wasizo sihitaji.
Agizo hilo amelitoa leo Juni 1,2022 jijini Dodoma wakati akipokea taarifa ya tathmini ya hali ya mawasiliano pamoja na hatua mbalimbali zilizochukuliwa kufuatia malalamiko ya watumiaji wa huduma za kampuni ya simu ya Vodacom Tanzania.
Waziri Nape amesema kuwa mnatakiwa kutatua kero na malalamiko ya wananchi kuhusu huduma za mawasiliano pamoja na kuangalia namna ya kuwawezesha watanzania kuongeza matumizi ya simu janja
“Maagizo yangu kwa makampuni ya simu yote nchini na TCRA mtafute njia ambayo itasaidia kukomesha malalamiko ya wateja kuunganishwa na huduma wasizo zihitaji na kuendelea kukatwa fedha hii tukomeshe mara moja”amesema Nape
Hata hivyo amesema kuwa siyo jambo la busara Kampuni za simu kuendelea na tabia ya kuunganisha wateja katika huduma wasizo zihitaji bila ridhaa yao.
“Kila mtoa huduma ya mawasiliano aende kwa wateja wake pamoja na wadau wanaowasaidia kutoa huduma kwa wananchi ili wasikilize malalamiko na kuyatatua ,haiwezekani Serikali pekee ndio iwe inasikiliza na nyie makampuni ya simu ina wajibu wa kufanya hivyo”.
Waziri Nape ameilekeza TCRA na makampuni ya simu kukaa na kutatua malalamiko ya matumizi ya bando ambayo mtumiaji hajui limetumikaje ambapo ameelekeza makampuni ya simu kuboresha program tumizi (mobile application) ili iwe rahisi kuisoma na itoe taarifa nyingi zaidi ili kupunguza malalamiko ya watu kutojua wametumiaje data zao
“Matumizi ya bado yamekuwa yakilalamikiwa sana na wananchi hivyo makampuni ya simu pamoja na TCRA mtafute program hiyo tumizi ambayo itamwezesha hata mwananchi wa chini kuwa na uwezo wa kusoma kiasi cha bado ambacho amekitumia ili kuondo malalamiko”amesema
Waziri Nape ameitaka TCRA na makampuni ya simu kuona namna ya kumsaidia kila mtanzania kumiliki na kutumia simu janja kwa kuangalia namna ya upatikanaji wa simu janja kwa bei nafuu na ikiwezekana ufanyike utaratibu wa mwananchi kununua simu kwa mfumo wa kulipia kwa awamu ndani ya mwaka mmoja au miwili ili kuongeza matumizi ya intaneti nchini
“Ikumbukwe kuwa Serikali iliondoa kodi kwenye simu janja lakini takwimu zinaonesha matumizi ya simu janja yameongezeka kwa asilimia mbili tu, kwa kuwezesha wananchi kutumia simu janja itaongeza watumiaji wa huduma ya intaneti, makampuni mtapata fedha Serikali itaongeza mapato na mwananchi atapata huduma anayostahili”,
Hata hivyo Waziri Nape ameipongeza Kampuni ya Vodacom Tanzania kwa kuwa wa kwanza kwenda kufanyia kazi malalamiko ya wananchi na kuyashauri makampuni mengine kutekeleza hilo huku akiwashukuru wote waliowekeza katika sekta ya mawasiliano na kuwahakikishia kuwa Serikali inaendelea kushirikiana na sekta binafsi ili kumhudumia mtanzania
Kwa upande wake Mkurugenzi wa masuala ya kisekta Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Dk. Emmanuel Manase,amesema kuwa lengo la serikali ni kuboresha huduma za mawasiliano nchini.
Dk. Manase amesema kuwa Serikali ilitoa maagizo kwa Kampuni za simu kufanyia kazi malalamiko ambayo imekuwa ikiyapokea kutoka kwa wanchi ili kuboresha utoaji huduma.
Awali, Mkurugenzi Mkuu wa Vodacom Tanzania, Sitholizwe Mdlalose,amesema kuwa wametekeleza maagizo yaliyotolewa na serikali kwa kuwatembelea wadau wao katika maeneo mbalimbali na kubaini kero zinazowakabili na kuzifanyia kazi.
Amesema kuwa Vodacom Tanzania inafanya kazi kwa ushirikiano na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) na kujenga minara ya mawasiliano 23 ili kupanua wigo wa mtandao wa simu kufikia asilimia 93 ya watu watanzania wanaopata huduma ya mawasiliano ya simu ikiwa pia ni sehemu ya kampeni ya kampuni hiyo ya kuiunganisha Afrika ambayo inatambua fursa za zinazotolewa na maunganisho ya kidijitali katika bara la Afrika
Ameongeza kuwa Kampuni hiyo ya simu ilifanya ukaguzi wa kina kwenye huduma zao zote za kidijitali zinazotolewa na mawakala wasimamizi, na kugundua baadhi ya changamoto ambazo zishughulikiwa na tayari simu za malalamiko kutoka kwa wateja zimepungua kwa asilimia 30