***************************
Na MWANDISHI WETU
Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) ukiambatana na baadhi ya wabunge ambao ni wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge, Katiba na Sheria wamekutana na wanachuo cha Uhasibu Arusha (IAA), kwa lengo la kutoa elimu ya hifadhi ya jamii na umuhimu wa kujiwekea akiba kupitia Mpango wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii kwa Sekta Isiyo Rasmi.
Katika kutoa elimu hiyo kuliambatana na burudani mbambali ikiwa ni pamoja na vichekesho kutoka kwa Zuli Comedy vilivyolenga kutoa elimu kuhusu hifadhi ya jamii.
Akizungumza katika kampeni hiyo, Meneja wa Sekta isiyo rasmi wa NSSF, Rehema Chuma, alisema Mfuko umelenga kutoa elimu ya hifadhi ya jamii kwa wanachuo hao ili waweze kutambua umuhimu wa kujiwekea akiba wakiwa chuoni na baadaye akiba hiyo iwe na manufaa kwao.
Kwa upande wao wabunge hao ambao ni wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge, Katiba na Sheria wakiwemo Mhe. Suma Fyandomo, Mhe. Joseph Tadayo na Mhe. Agnes Hokororo wote kwa nyakati tofauti walipata nafasi ya kuzungumza na wanafunzi hao ambapo kila mmoja alielezea namna alivyoona fursa na umuhimu wa kujiwekea akiba na NSSF.
Naye, Meneja wa NSSF Mkoa wa Arusha, Josephat Komba alisema kuna umuhimu mkubwa wa kujiwekea akiba NSSF.
Wanafunzi wa Chuo cha Uhasibu Arusha baada ya hamasa hiyo walijitokeza kwa wingi kujiunga na NSSF kupitia Mpango wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii kwa Sekta isiyo rasmi.