Meneja mauzo Kanda ya Mwanza kutoka Kampuni ya bia (TBL) Yuda Ryaga akizungumza na waandishi wa habari leo hii
Meneja mauzo Kanda ya Mwanza kutoka Kampuni ya bia (TBL) Yuda Ryaga akieleza namna ambavyo wanashirikiana na Jamii katika kuinuana kiuchumi
****************************
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Ikumbukwe kuwa maji ni uhai na nimuhimu katika kuendesha shughuli mbalimbali katika familia na Jamii kwa ujumla Kampuni ya Bia Tanzania (TBL)Mkoa wa Mwanza kwakulitambua hilo imeendelea kutoa huduma ya maji safi na salama kwa kata tano zilizoko katika Wilaya ya Ilemela.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Juni 1,2022 Meneja mauzo Kanda ya Mwanza kutoka katika Kampuni hiyo Yuda Ryaga, amesema TBL inatoa huduma ya maji safi na salama kwa kata hizo ambazo ni Pansiansi,Ilemela,Kirumba,Kitangiri,kilimahewa pamoja na taasisi mbalimbali za Serikali na zisizo za kiserikali.
“Tulipewa kibali na Wizara ya Maji na maji haya tunayavuta kutoka ziwani baada ya hapo tunayatibu na kuyachuja vizuri kwaajili ya matumizi ya kuzalishia bidhaa zetu na matumizi ya kunywa kwa wananchi pamoja na shughuli mbalimbali za nyumbani”,amesema Ryaga
Amesema Wananchi wanaanza kupata huduma ya maji safi na salama kuanzia saa 12 asubuhi hadi saa 12 jioni bila gharama yoyote kwani lengo lao ni kuisaidia jamii kuwa na uhakika wa kuyapata maji.
Katika hatua nyingine Ryaga amesema kuwa wanaendelea kuwasaidia wakazi wa Mkoa wa Mwanza kwa kutoa ajira za moja kwa moja na za muda lengo ni kuwainua kiuchumi.
Ameongeza kuwa Kampuni hiyo pia inatoa machicha ya mabaki ya bidhaa wanazozalisha kwa wafugaji ili mifugo iweze kupata chakula ambapo wanauza shilingi elfu mbili kwa tani moja.