****************************
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro amesema mfumo wetu wa haki jinai ni mzuri lakini kuna baadhi ya mambo yamepitwa na wakati ukilinganisha na uhalisia, hivyo ni vema mfumo uangaliwe upya kwa kushirikiana na wadau.
Dkt. Ndumbaro ameyasema hayo alipokutana na kufanya mazungumzo na wawakilishi wa Kituo Cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) ofisini kwake jijini Dodoma leo Juni 1, 2022.
Dkt. Ndumbaro alisema “Mfumo wa haki jinai unatusaidia lakini baadhi ya mambo yamepitwa na wakati”
Awali, Mwenyekiti wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) Bi. Anna Henga alisema ni muhimu Serikali ikafanya maboresho ya mfumo wa Haki Jinai kwani mfumo uliopo sasa unasababisha kesi kuchukua muda mrefu na mahabusu kulundikana.
Bi Henga alisema “Kuanzia Mwaka 2020 hadi 2022 mahabusu ni wengi kuliko wafungwa kwani mahabusu wengi hawapewi dhamana na hivyo kusababisha mlundikano magerezani”
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu ni kituo kikubwa zaidi kinachotoa msaada wa kisheria na kinahudumia watu sio chini ya 150 kwa siku, pia kina waangalizi wa haki za Binadamu wilaya zote nchini.