Meneja wa NEMC Kanda ya kaskazini , Lewis Nzali akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake katika kuelekea siku ya mazingira duniani Juni 5 ,mwaka huu.(Happy Lazaro)
************************
Happy Lazaro,Arusha.
Arusha.Wachimbaji wa madini ujenzi ikiweko moramu,kokoto na vifusi wametakiwa kufanya shughuli zao kwa kufuata sheria na taratibu za Baraza la Taifa la hifadhi na usimamizi wa mazingira (NEMC) kwani inawezekana kabisa kuchimba bila kuwepo majanga yoyote.
Hayo yamesemwa leo jijini Arusha na Meneja wa NEMC Kanda ya kaskazini,Lewis Nzali wakati akizungumza na waandishi wa habari katika kuelekea maadhimisho ya siku ya mazingira duniani ambayo hufanyika June 5 kila mwaka .
Amesema kuwa,katika kuelekea maadhimisho hayo wamekuwa wakifanya shughuli mbalimbali ikiwemo kutoa elimu kwa jamii kuhusiana na umuhimu wa kutunza mazingira sambamba na upandaji miti.
Amesema kuwa, kumekuwepo na uchimbaji holela wa madini ujenzi ambao umekuwa ukifanywa bila kufuata sheria na taratibu za NEMC ambazo mwisho wa siku huleta maafa na majanga makubwa kwa jamii ikiwemo vifo.
Nzali amesema kuwa, wachimbaji hao inawezekana kabisa kuchimba bila kutokea maafa endapo watafika ofisi za NEMC na kuweza kuelekezwa namna ya kufuata utaratibu wa kimazingira.
“Tunafahamu wazi namna ambavyo uchimbaji holela usiozingatia sheria na kanuni unavyoleta maafa kwa watu huku wengi wao wakipoteza maisha kutokana na uchimbaji huo,hivyo tumekuwa tukitoa elimu kwa wachimbaji na wamiliki katika kuzingatia uchimbaji salama unaofuata sheria na taratibu za NEMC.”amesema.
Ameongeza kuwa,swala la kutunza mazingira ni la kila mmoja wetu,ambapo wamekuwa wakitoa elimu hiyo kuanzia ngazi za chini wakiwemo wanafunzi ambao wamekuwa waalimu wa wenzao katika kuhakikisha mazingira yanalindwa na kutunzwa ipasavyo.
“Katika kuelekea kilele cha siku ya mazingira duniani Juni 5,tunashirikiana na wadau mbalimbali kupanda miti katika maeneo mbalimbali sambamba na usafishaji wa mito ambapo kwa kufanya hivyo tumeweza kutunza mazingira na kuhakikisha yanakuwa salama muda wote”amesema.
Hata hivyo amewataka wadau kuchangamkia fursa ya kusajili na kuunda vikundi vya mazingira na kuingia makubaliano na jiji la Arusha katika kutunza mazingira kama wanavyofanya jiji la Moshi kwani ni fursa kubwa Sana na inaweza kuchangamkiwa.
Amesema kuwa, kauli mbiu ya kitaifa kwa mwaka huu ni”Tanzania ni yetu tutunze mazingira huku kauli mbiu ya kidunia ikiwa ni “dunia ni moja tu hivyo tuitunze ambapo maadhimisho hayo kitaifa yatafanyika mkoani Dodoma .