Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini Mhe. Jabir Shekimweri (aliyeva kofia nyekundu) akitoa maelekezo kwa Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Miliki na Majengo Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACF) Salum Mohamed (kushoto), alipotembelea mradi wa ujenzi wa Kituo cha Zimamoto na Uokoaji Nzuguni jijini Dodoma leo tarehe 31 Mei, 2022.
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini Mhe. Jabir Shekimweri akisaini kitabu cha wageni alipotembelea ofisi ya Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji baada ya kufanya ziara katika mradi wa ujenzi wa Kituo cha Zimamoto na Uokoaji Nzuguni jijini Dodoma leo tarehe 31 Mei, 2022.
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini Mhe. Jabir Shekimweri (mwenye shati la kijani) akiwa na Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya ya Dodoma Mjini kwenye picha ya pamoja na Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji John Masunga (kulia kwake) na Kamishna wa Utawala na Fedha wa Zimamoto na Uokoaji Mbaraka Semwanza, ndc (kushoto kwake)
***************************
Dodoma 31 Mei, 2022
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini, Mhe. Jabir Shekimweri, leo tarehe 31 Mei, 2022 amefanya ziara katika mradi wa Ujenzi wa Kituo Cha Zimamoto na Uokoaji kilichopo Nzuguni kitakachotoa huduma kwa wananchi wa Nzuguni na maeneo jirani na kuhitimisha ziara yake kwa kumtembelea Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Makao Makuu ya Zimamoto na Uokoaji jijini Dodoma.
Akiambatana na Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya ya Dodoma, Mheshimiwa Shekimweri ameipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuliwezesha Jeshi hilo kufikisha huduma zake katika ngazi za wilaya ili kuweza kukabiliana kiurahisi na matukio ya Moto na Maokozi mbalimbali.
“Naipongeza Serikali yetu sikivu kwa kuliwezesha Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kuweza kuwafikia wananchi kwa ngazi za Wilaya, Mfano mzuri ni kituo hiki kilichojengwa hapa Nzuguni” alisema Mhe. Shekimweri baada ya kupata maelezo ya ujenzi huo kutoka kwa wasimamizi wa Ujenzi.
Mhe. Shekimweri pia aliwasiliana na Meneja wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Mkoa wa Dodoma na kumuomba uwezekano wa kufikisha barabara kwa uharaka katika Kituo hicho kinachotazamiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Juni, 2022.
Mhe. Shekimweri alimalizia Ziara yake kwa Kumtembelea Kamishna Jenerali wa Jeshi hilo John Masunga na kupokelewa katika Ofisi zake zilizopo Makao Makuu ya Jeshi hilo Jijini Dodoma. Kamishna Jenerali Masunga, akimkaribisha Mkuu huyo wa Wilaya alimpongeza kwa jitihada binafsi anazozifanya kwa Jeshi lake na kuahidi kuyachukua yote aliyoyashauri ili kuendelea kuimarisha utendaji kazi.
Kamishna Jenerali Masunga alimuahidi Mkuu wa Wilaya kuwa, askari na maafisa wake wataendelea kutoa elimu ya kinga na tahadhari dhidi ya majanga ya moto na maokozi kwa wananchi ili kupunguza idadi ya matukio katika maeneo mbalimbali.