***********************
Wakazi zaidi ya 40,000 wa tarafa ya Liganga wanatarajia kuondokana na adha ya kutembe umbali mrefu wa zaidi ya km. 50 kwenda kufuata huduma ya afya kutokana na ujenzi wa kituo cha afya unaoendelea katika kata ya Mundindi kufikia hatua za mwisho.
Akizungumza mara baada ya mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga kuwasili katika kituo hicho akiwa ameongozana na viongozi wa Chama cha Mapinduzi na Serikali Afisa mtendaji wa kata ya Mundindi Tumaini Ng’ande amesema ujenzi wa kituo hicho ulianzishwa kwa nguvu za wananchi ndipo serikali ikaunga mkono juhudi hizo za wananchi kwa kutoa fedha kiasi cha Sh. Milioni 500 huku nguvu kazi ya wananchi ikiwa ni zaidi ya Milioni 89.
“Serikali imetupa Milioni 500 ambazo zilitolewa kwa awamu mbili, milioni 250 kwa awamu ya kwanza na milioni 250 kwa awamu ya pili. Katika fedha za awamu ya kwanza tumebakiwa na sh. Milioni 73 na hizi za awamu ya pili hatujazigusa na zote zipo kwenye akaunti kwaajili ya kuendeleza ujenzi wa jengo la mama na mtoo, nyumba ya mganga na sehemu ya kufuli”,
Aidha kwa upande wake Diwani wa Kata hiyo ambaye pia ni mwwenyekiti wa Halmashauri hiyo ya Ludewa Wise Mgina amesema wanatarajia mpaka kufikia Juni 30 mwaka huu watakuwa wamekamilisha ujenzi huo hivyo kwa sasa jengo la utawala, OPD, kichomea taka pamoja na maabara tayari yamekwisha kamilika huku katibu wa Chama cha Mapinduzi Amos Kusakula akiwasihi kununua malighafi za ujenzi mapema ili kuepuka mfumoko wa bei pindi unapotokea.
Joseph Kamonga ni mbunge wa jimbo hilo amesema fedha za tozo ndizo zilizotolewa katika ujenzi huo na kuahidi kufuatilia vifaa hivyo ili viweze kupatikana kwa wakati na wananchi hao waanze kupata huduma mapema.
“Jambo hili nimesha lisemea bungeni, lakini pia nitaendelea kulisemea ili tupate vifaa kwa haraka, pia nitaiomba serikali iweze kutupatia gari la wagonjwa ili iwe rahisi kuhudumia wagonjwa wa tarafa nzima kwakuwa wananchi wa kata ya Mavanga, Madilu na kwingineko wanatarajia kupata huduma katika kituo hiki”.
Sanjali na hilo pia amewapongeza viongozi wanaosimamia ujenzi wa zahanati hiyo, kwa kuijenga katika ubora na kufanya kazi hadi nyakati za usiku ili kukamilisha kwa wakati.