- Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini – Wizara ya Afya Bi. Catherine Sungura akifafanua jambo kwa waandishi wa habari mara baada ya kufanya ziara ya kutembelea miradi ya ujenzi inayoendelea kufanyika katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mawenzi, Kilimanjaro.Kaimu Mganga Mfawidhi katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mawenzi, Kilimanjaro Dkt. Jonas Kessy akisema jambo kwa waandishi wa habari kuhusu miradi ya ujenzi inayoendelea katika Hospitali ya Mawenzi.Jengo la Huduma za Dharura katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mawenzi, Kilimanjaro ambalo limekamilika kwa asilimia 95 huku tayari huduma zikiwa zimeanza kutolewa. Ujenzi wa jengo hili umegharimu kiasi cha Milioni 764.Jengo la Huduma za Mama na Mtoto katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Mawenzi, Kilimanjaro ambapo ujenzi wake umefikia hatua ya nane sasa.
*******************
Na. WAF-Moshi.
Serikali kupitia Wizara ya Afya imewekeza fedha kwa ajili ya kuboresha miundimbinu ya kutolea huduma za afya ikiwemo hospitali za rufaa za mikoa ambapo Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mawezi (Kilimanjaro) imeweza kutekeleza mradi wa ujenzi wa jengo la mama na mtoto.
Hayo yamebainishwa na Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini kutoka Wizara ya Afya Bi. Catherine Sungura wakati alipotembela miradi inayotekelezwa na Serikali kwenye hospitali hiyo.
Bi. Sungura amesema kuwa Serikali imetoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa jengo la mama na mtoto katika hospitali hiyo ambapo ujenzi wake unaendelea vizuri na kwa sasa imefikia awamu ya nane ya ujenzi huo na kiasi cha shilingi bilioni 4 zimekwishatiolewa kwa ajili ya kutekeleza awamu hiyo.
“Kukamilika kwa ujenzi wa jengo hili litasaidia kupunguza vifo vya mama na mtoto vitokanavyo na uzazi, jengo hili litakua na huduma zote zinazohitajika katika kila wodi na pia kwa upande wa wagonjwa wa nje mama na mtoto ataweza kupata huduma zote hapa hapa” amefafanua Bi. Sungura.
Ametaja mradi mwingine katika hospitali hiyo ni ule wa ujenzi wa jengo la huduma za dharura ambapo jengo hilo limekamilika kwa asilimia 95 huku tayari huduma za afya zikianza kutolewa katika jengo hilo lililogharimu zaidi ya shilingi milioni 764 ambalo pia litawekewa vifaa vya kisasa.
Kwa upande wa Jengo la wagonjwa mahututi Bi. Sungura amesema Serikali imetoa kiasi cha shilingi milioni 149 kwa ajili ya ukarabati wa jengo hilo na hadi sasa utekelezaji huo umefikia asilimia 80.
Naye Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo Dkt. Jonas Kessy amesema kukamilika kwa jengo la Mama na Mtoto kutasaidia kuondoa msongamano katika wodi ya wanawake na watoto na hivyo ameishukuru Serikali kwa uwekezaji mkubwa ambao umefanyika katika hospitali hiyo.
Baadhi ya wananchi wa mkoa wa Kilimanjaro wameishukuru Serikali kwa kuendela kuboresha miundombinu ya Afya ambapo Bw. Marco Sambo ameipongeza Serikali kwa kutoa fedha hizo ambazo zimesaidia kuboresha huduma katika hospitali ya Mawenzi na hivyo kuwaondolea msongamano na kuwapunguzia muda wa kupata huduma.
Kwa upande wake Bi. Anitha Juma alisema kuwa ameridhika na maendeleo ya ujenzi na ukarabati wa hospitalinini hapo na kikubwa alichokipenda ni kupungua kwa misongamano wakati wa kupata huduma.