*****************************
NJOMBE
Wakala wa barabara za vijijini na Mijini TARURA mkoani Njombe umekamilisha ujenzi wa daraja linalounganisha kata za Ramadhani na Njombe mjini uliyogharimu zaidi ya mil 986 na kisha kukomesha changamoto ya madereva wa vyombo vya moto na wafafunzi kutumbukia mtoni katika kipindi cha masika.
Wakizungumzia kukamilika kwa daraja hilo ambalo limevuka muda wa ujenzi kimkataba ,Wakazi wa kata ya Ramadhani na Njombe mjini wakiwemo Wafanyabiashara wadogo na madereva bodaboda wanasema awali eneo hilo lilikuwa na daraja la matapa jambo ambalo lilikuwa likihatarisha usalama kwa watumiaji
Wamesema kuna nyakati maji yalifunika darala hilo hatua ambayo ilisababisha vyombo vya moto kusombwa na mto huku wanafunzi wanaosoma shule ya sekondari Mabatini na Shule ya Msingi Ruhuji wakilazimika kuzunguka umbali mrefu wakikwepa kuvuka katika eneo hilo hatarishi.
Mbali na kuondokana na adha hiyo wakazi hawa wanasema kufunguka kwa mawasiliano katika kata hizo mbili kumechagiza kasi ya ukuaji wa biashara kwakuwa wakulima wanatumia njia hiyo kupeleka mazao mjini.
Mhandisi Gerard Matindi ambaye ni Meneja wa TARURA mkoa wa Njombe anasema licha ya kusuasua kipindi cha nyuma kutokana na mvua nyingi zilizokuwa zinanyesha mkoani Njombe lakini sasa ujenzi umekamilika kwa asilimia 100 hivyo wananchi wanakwenda kusahau shida walizokuwa wanakumbana nazo awali.
Katika hatua nyingine amezungumzia kuanza ujenzi wa miradi ya barabara ya Nazareth Center na Lutilage hadi joshoni kwa kiwango cha rami na unaotekelezwa na kampuni ya kizalendo ya GS Contractor ambao utakaogharimu zaidi ya bil 1.8