*******************************
Na Mwandishi wetu, Simanjiro
SHIRIKA lisilo la kiserikali la ECLAT Foundation limekabidhi madarasa saba yakiwemo matatu mapya na manne yaliyokarabatiwa ya shule ya msingi Nakweni ya Kata ya Shambarai Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara.
Pia, ECLAT Foundation, imekabidhi madawati 69, ofisi mbili za walimu, viti 12 na meza 12 ambapo thamani ya miradi hiyo ni shilingi milioni 162.
Mwenyekiti wa ECLAT Foundation, Peter Toima akizungumza baada ya kukabidhi mradi huo amesema baada ya kuelezwa changamoto ya upungufu wa madarasa waliamua kuyafanyia kazi.
Amesema shirika la ECLAT Foundation limefanya mambo mengi kwa ajili ya manufaa ya jamii japokuwa hawajigambi wala kutamba kwani wanasaidia wananachi.
“Sisi na shirika la Ujerumani la Upendo tulipopata taarifa ya mapungufu ya shule hii tuliweka mikakati na kufanikisha ujenzi wa miundombinu hii,” amesema Toima.
Mkuu wa wilaya ya Simanjiro Dk Suleiman Serera amewapongeza wana Kijiji wa Nakweni kwa kuanzisha mradi huo kwani endapo wasingeanzisha ECLAT wasingeumaliza na kujenga mingine.
Hata hivyo amewataka wanafunzi, walimu, wazazi na walezi wa shule hiyo kutunza miundombinu hiyo kwa ajili ya manufaa yao.
“Baada ya mradi huu kukabidhiwa kwenu mnapaswa kuitunza kwani wakati wa ukaguzi nimeona darasa moja limechorwa na wanafunzi,” amesema Dk Serera.
Mwalimu mkuu wa shule hiyo Namweli Chao amesema shule hiyo ilianzishwa baada ya wanafunzi wa kijiji hicho kutembea umbali mrefu kufuata elimu maeneo mengine.
“Wanafunzi walikuwa wanatembea kilomita 22 hadi kijiji cha Kilombero au kilomita 18 kwenye kijiji cha Olbili kwenda kusoma kwenye shule za msingi na kurudi kwa kilomita hizo,” amesema Chao.
Mwanafunzi wa darasa la sita wa shule ya msingi Nakweni, Esupati Ngidutu amesema awali wanafunzi wa madarasa mawili walikuwa wanatumia chumba kimoja kusoma.
Mwanafunzi wa darasa la tano wa shule hiyo Saruni Ikoyo amemshukuru Toima Mwenyekiti wa ECLAT Foundation kwa kufanikisha ujenzi wa madarasa hayo.