Na. Damian Kunambi, Njombe
Mbunge wa jimbo la Ludewa, Joseph Kamonga ametembelea mradi wa ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) kinachojengwa katika kata ya Lugarawa Wilayani Ludewa Mkoani Njombe kitakacho gharimu kiasi cha zaidi ya Sh. Bilion 5.
Akiwa katika mradi huo sambamba na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi na Serikali Kamonga Amesema wananchi wa Ludewa na mkoa wa Njombe kwa ujumla wanauhitaji mkubwa wa chuo hicho na ndiomaana akakisemea bungeni ili aweze kupata fedha za kuendeleza ujenzi huo.
“Chuo hiki kilianza kujengwa mwaka 2005, lakini hakikuendelea na kikaishia kuchimbwa msingi hivyo wananchi walivyonipa dhamana ya kuwaongoza nikaona nianze na vipaumbele vyao ikiwemo Chuo hiki cha Veta”.
Ameongeza kuwa fedha hizo zilizotolewa na serikali zinatosheleza kukamilisha ujenzi huo pamoja na kununua vifaa vya kufundishia hivyo kwa sasa wao kama viongozi wanafanya ukaguzi wa mara kwa mara ili kuhakikisha ujenzi huo unaendana na thamani ya fedha iliyotolewa.
Amos Kusakula ni katibu wa CCM wilaya ya Ludewa amewataka wasimamizi wa mradi kuwa wazalendo na kuhakikisha kila kitu kinafanyika kwa ubora kwakuwa mradi huo una manufaa kwa watanzania wote kwa ujumla.
“Hiki chuo si kwa manufaa ya wakazi wa Njombe na Ludewa pekee, bali wanufaika ni watanzania wote! Hivyo msije kufanya kazi kwa kuripua mkiamini kwenu haitawapa hasara yoyote, hapo mtakuwa mmejidanganya wenyewe”.
Aidha kwa upande wa Mhandishi kutoka wizara ya Elimu Issa Shebe amesema mradi huo mpaka sasa ulitakiwa kukamilika kwa 40% lakini kutokana na changamoto mbalimbali kwasasa umekamilika kwa 20% pekee.
Ujenzi wa mradi huo ulisimama kwa takribani miaka 15 ukiwa katika hatua ya msingi ambapo kwa sasa ujenzi huo unaendelea kwa kasi na kukamilika kwake itakuwa ni mkombozi mkubwa kwa wakazi wa Ludewa na mkoa wa Njombe kwa ujumla.