Mratibu wa Masuala ya Jamii MEWATA, Dkt. Asha Mahita
Mratibu wa Masuala ya Jamii MEWATA, Dkt. Asha Mahita akimpongeza Mkurugenzi wa Hinatas Foundation, Ayshat Sanya kwa kujitolea kwa jamii
Mkurugenzi wa Hinatas Foundation, Ayshat Sanya akimkabidhi Mkuu wa Shule ya Sekondari Kinyamwezi, Sifa Mwaruko na baadhi ya wanafunzi maboksi yenye taulo za kike, zilizotolewa na Taasisi hiyo anayoisimamia pamoja na Taasisi mwenza ya Iseland, mapema hii leo
Kiongozi wa Taaluma Kinyamwezi Sekondari, Rahma Mwalimu akisoma risala
Wanafunzi wa kidato cha nne wakionesha igizo lenye maudhui ya kuelimisha jamii kuhusu hedhi salama
***************************
Na Veronica Mrema
Vijana wa kike na wa kiume zaidi ya 1,000 wa Shule ya Sekondari Kinyamwezi wamepatiwa elimu kuhusu hedhi salama na Wataalamu mabingwa kutoka Chama cha Madaktari Wanawake Tanzania {MEWATA}.
Sambamba na hilo, shule hiyo imekabidhiwa taulo za kike 1,000 zilizotolewa na Taasisi isiyo ya Kiserikali ya Hinatas Foundation pamoja na Iseland Foundation ikiwa ni sehemu ya kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Hedhi Duniani ambayo hufanyika Mei 28, kila mwaka.
Akizungumza, Kiongozi wa Taaluma shuleni hapo, Rahma Mwalimu {kidato cha pili}, ameshukuru taasisi hizo kuwapatia taulo hizo kwani zitasaidia baadhi ya wasichana ambao hushindwa kuhudhuria masomo yao wanapokuwa katika kipindi hicho.
“Kuna wengine wanatoka mazingira magumu, mtu kwao mwengine hana uwezo wa kununua pedi… wengine tunaweza … mtu akitoka kwao anajua labda vifaa vinaletwa {taulo za kike} na vingine lakini akifika hamna,.. inakuwa changamoto kwa mtoto wa kike,” amesema.
Amesema kutokana na changamoto ambazo wasichana hupitia waliamua kuanzisha klabu maalum ya wasichana jitambue ili kuzidi kuelimishana wao kwa wao.
“Inatusaidia kujitambua na kujielewa, uwe msafi vipi, namna gani utunze mazingira, kutunza ile sehemu ya kutupa pedi, usitupe pedi hovyo kwa sababu zile damu zinazotoka ni uchafu,” amesema.
Naye, Juma Abdul amesema jamii inapaswa kumthamini na kumpa ushirikiano thabiti msichana ili ajisikie fahari kuzaliwa na jinsi ya kike na hususan pale anapokuwa katika kipindi cha hedhi
“Ili asijisikie vibaya hasa katika kipindi cha hedhi, apewe elimu na jamii iwe na elimu kuhusu hedhi, wazazi wakae na watoto na wawaeleweshe pia kuhusu masuala ya utandawazi.
“Wawaeleze ile {hedhi} ni sifa ambayo Mungu kampatia mwanamke, ni kheri ajivuni, ajikubali na kuona Mungu kamjalia, elimu inahitajika kwenye jamii,” amesema.
Ameongeza “ni muhimu pia kuwepo na uhusiano mzuri kati ya wasichana na walimu wa kike ili pale wanapohitaji usaidizi na ushauri na elimu waweze kusaidiwa kwa wakati.
Akizungumza na wanafunzi hao, Mratibu wa Masuala ya Jamii MEWATA, Dkt. Asha Mahita amewahimiza wasichana kuzingatia usafi wanapokuwa katika kipindi cha hedhi ili wasipate maradhi.
“Hili somo la hedhi limekuja kwa uelewa, watoto wa kike wajue jinsi gani wanapokuwa kwenye hedhi anatakiwa afanye kitu gani na ajikinge na nini.
Ameongeza “Kwa sababu ukiwa mchafu utapata maradhi na sisi tunakukinga usipate maradhi kwa kukupa elimu.
“Mtoto wa kike ukipevuka, ina maana wewe saa yoyote unaweza kupata ujauzito na anayekupa uajauzito ni mtoto wa kiume.
“Tumeshuhudia wanafunzi wawili wamepeana ujauzito matokeo yake wote wamefukuzwa shule, hawawezi kuendelea,” amesema.
Amewahimiza vijana hao kuzingatia masomo wanayofundishwa na walimu wao darasani pamoja na kuwatii wazazi/walezi wao kwenye jamii ili waweze kuzifikia ndoto zao.
Mkuu wa Shule hiyo, Sifa Mwaruka amesema “Tumefurahia mno… tunashukuru mno Hinatas na Island ambao wamekuja pamoja na foundation zote ambazo zimeambatana nazo.
“Wametupa moyo, wametu-support, wametupa furaha, tumefurahi kwa sababu wangeweza kwenda shule nyingine mjini, lakini wamekuja kwetu.
“Wasichana wamefurahi sana kwa sababu huwa wanapata shida wengi wametoka familia duni, unakuta mwingine anaweza akapata hedhi na akakosa kuja shuleni kwa sababu hana kitu cha kujihifadhi.
“Akitumia kitambaa unakuta hedhi imekuja nyingi kwa hiyo anaogopa kuchafua sketi yake. Kwa hiyo anabaki nyumbani mpaka siku tatu zitakapoisha au atakapomaliza mzunguko wake ndiyo anakuja shuleni,” amesema.
Amesema taulo hizo walizokabidhiwa zitachochea hamasa kwa wanafunzi kuhudhuria masomo kwani wale ambao hawana uwezo wa kununua, watapatiwa.
“Itafanya sasa waje shuleni, vitu hivi vya kujihifadhi vipo na tunamshukuru Mungu vyoo vyetu vya shimo hivyo, akitumia atatupa humo,” amesema na kubainisha shule hiyo ina taribani wanafunzi 1,900 na wamekuwa wakijpambana kuitahidi kitaaluma.
“Tunaenda nao…, mwaka jana wanafunzi 55 kati ya 320 waliofanya mtihani wameenda kidato cha tano na wengine wameenda chuo, division one tulipata nne, two 22, there kama 50.
“Tunamshukuru Mungu tunavyoendelea, kitu kikubwa sana mazingira ya shule yanawafanya wawe ‘confotable’ kusoma,” amesema.