*************************
Na Mwandishi wetu, Hanang’
MBUNGE wa Jimbo la Hanang’ Mkoani Manyara, mhandisi Samwel Xadhay Hhayuma amejitolea mabati 100 kwa ajili ya kuezeka ofisi ya CCM Kata ya Laghanga.
Mhandisi Hhayuma akizungumza wakati akikabidhi mabati hayo amesema lengo ni kuhamasisha kata nyingine zisizo na ofisi za CCM kuzijenga.
“Ni imani yangu tumeshikana mikono ili kuchochea wanachama wa CCM wengine wahamasike ili ofisi za CCM zing’are kama ofisi za serikali zinavyong’ara, amesema.
Mjumbe wa kamati ya siasa ya CCM kata ya Laghanga, Salim Jula amempongeza mhandisi Hhayuma kwa kutimiza ahadi yake aliyoitoa ya kuwapa mabati 100 ya kuezeka ofisi.
“Tunampongeza mbunge Hhayuma kwa kutukabidhi mabati haya ambayo yatanufaisha wanachama kwa kukaa kwenye ofisi nzuri tofauti na awali,” amesema Jula.
Diwani wa kata ya Laghanga, Emmanuel Ngora amemshukuru mbunge huyo kwa kuwapatia mabati 100 kwa ajili ya ujenzi wa ofisi ya CCM ya kata hiyo.
“Kwa niaba ya wanachama wa CCM wa kata ya Laghanga tunamshukuru mbunge wetu kwa kutuwezesha mabati 100 ya upauzi wa ofisi yetu,” amesema Ngora.