**************************
Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Bi. Mary Makondo amezindua rasmi Kamati ya Mkoa ya Uratibu wa Wadau wa Huduma za Msaada wa Kisheria kwa mkoa wa Pwani. Uzinduzi huo umefanyika leo, Mei 27, 2022, Mkoani Pwani.
Bi. Makondo amewasihi wajumbe wote wa Kamati hii kuzingatia na kutekeleza majukumu yao kwa weledi na uadilifu kama ilivyoainishwa kwenye Mwongozo wa Uundaji wa Kamati hizi za Mikoa.
“Kwa kuwa ninyi ndio waratibu wa huduma ya msaada wa kisheria kwa Mkoa huu wa Pwani, msisite kuchukua hatua za kinidhamu kupitia mamlaka husika kwa Mashirika au Wasaidizi wa Kisheria watakaokiuka taratibu na Kanuni za Sheria ya Msaada wa Kisheria” alisema Bi. Makondo
Aidha, Bi. Makondo amesema, ili kufikia malengo tarajiwa ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya msaada wa kisheria, kuna kila sababu ya kuimarisha mawasiliano na ushirikiano wa karibu baina ya Kamati na Serikali, watoa huduma ya msaada wa kisheria, na wadau mbalimbali wa ndani na nje ya Nchi.
Pia amesema ni muhimu kushirikisha jamii katika mnyororo mzima wa upatikanaji haki kwani vitendo vingi vya ukatili hususani kwa wanawake na watoto vinafanywa na watu wa karibu ndani ya familia zetu. Kupitia Kamati hii, Bi. Mary Makondo amewataka wajumbe wakawe washauri wema wa kupinga dhuluma, unyanyasaji na vitendo vyote vya ukatili kupitia mifumo mbalimbali iliyopo kuanzia ngazi ya kijiji/mtaa hadi taifa.
“Natoa wito kwenu, kutumia vikao hivi vizuri na kuleta matokeo, ikiwa ni pamoja na kutumika kama jukwaa mojawapo la kuimarisha huduma za utoaji wa huduma za msaada wa kisheria katika mkoa wetu wa Pwani” alisema Bi. Makondo.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhe. Abubakar Kunenge amesema watendaji wa Mkoa wa Pwani wako tayari kwa kazi ya kusaidia wananchi na watatoa ushirikiano katika kufanikisha kazi ya Kamati ya Uratibu wa Wadau wa Huduma za Msaada wa Kisheria mkoani Pwani.
Katika kuimarisha utekelezaji wa Sheria ya Msaada wa Kisheria na Kanuni zake, Wizara imeweka mfumo wa usajili wa watoa huduma ya msaada wa kisheria; kuanzisha Kamati za Uratibu wa Msaada wa Kisheria kwa Mikoa 25 mpaka sasa; kuanzisha Dawati la Huduma ya Msaada wa Kisheria Mahakamani ambapo mpaka sasa madawati hayo yameanzishwa kwenye Vituo Jumuishi sita vya Utoaji Haki ikiwemo mkoani Dar es Salaam (Kinondoni na Temeke), Arusha, Mwanza, Morogooro na Dodoma.