Asila Twaha , TAMISEMI
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Jenista Mhagama amewataka maafisa utumishi kushughulikia changamoto za watumishi ili kuepuka malalamiko.
Waziri Mhagama ameyasema hayo Mei 26, 2022 Jijini Dodoma wakati akifungua kikao kazi cha Wakuu wa Idara/Vitengo vya Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu katika Utumishi wa Umma kutoka katika Wizara, Taasisi, Vitengo, Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa.
Akieleza malalamiko mengi ya watumishi inaonesha wazi kuwa baadhi ya maafisa kutotekeleza majukumu yao na hupelekea kuwepo kwa changamoto nyingi za utumishi.
“Maafisa utumishi ni kama walezi na ndio maana kada hii ipo sehemu nyingi sisi ni tunashughulikia rasilimaliwatu tunapaswa tujue wajibu wetu” amesema Waziri Mhagama
Ameeleza wapo baadhi ya maafisa utumishi ambao wanashindwa kushughulikia changamoto za kiutumishi na hupelekea kuisababishia Serikali kupata hasara, amesisitiza Serikali inaendeshwa kwa kuangalia uwajibikaji, utendaji kazi hivyo, ni wajibu wenu kusimamia sheria, kanuni, taratibu na miongozo ya utumishi wa Umma.
“Maafisa utumishi kushindwa kuingiza taarifa za kiutumishi sahihi ni dhahiri kuwa, unataka kuisababishia Serikali hasara kwa kuingiza watumishi ambao waliokwisha maliza utumishi wao ambao hawapo kwenye utumishi” amesisitiza Waziri Mhagama
Awali Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Prof. Riziki Shemdoe amewataka Maafisa Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu wa Malaka za Serikali za Mitaa kushughulikia kero za kiutumishi amesema kikao hicho watakapo maliza kitawasaidia kuleta mabadiliko katika utekelezaji wa kazi zao.
“ Watumishi wengi wapo Mamlaka za Serikali za Mitaa ambapo watumishi hao ndio wanawahudumia wananchi maafisa utumishi tekelezeni wajibu wenu wa kazi kwa kutenda haki na kufuata sheria na taratibu za kazi. amesema Prof. Shemdoe
Aidha, baadhi ya washiriki waliweza kupatiwa tuzo kwa kuthamini na kutoa mchango wa kufanikisha kikao hicho.
Kikao hicho cha Wakuu wa Idara/Vitengo vya Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu katika Utumishi wa Umma kitahitimishwa na kufungwa tarehe 27 Mei, 2022 mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Innocent Bashungwa