***********
Na Lilian Lundo – MAELEZO
Idara ya Habari (MAELEZO) na Vyombo vya Habari hapa nchini vimeagizwa kutoa elimu ya sensa ya watu na makazi inayotarajiwa kufanyika Agosti 23 mwaka huu, ili wananchi waweze kuelewa lengo na faida ya sensa hiyo kwao binafsi na kwa Taifa.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari,Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mohammed Abdulla ametoa agizo hilo leo Mei 27, 2022 katika mkutano wa wamiliki wa vyombo vya habari kuhusu maandalizi ya sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 uliofanyika kituo cha mikutano cha kimataifa cha Julius Nyerere, Jijini Dar es Salaam.
*“Naiagiza Idara ya Habari (MAELEZO) kushirikiana na ofisi ya Takwimu pamoja na Wanahabari kutoa elimu ya sensa kwa Watanzania ili waweze kutoa taarifa sahihi wakati wa kuhesabiwa,”* alifafanua Naibu Katibu Mkuu.
Aliendelea kusema kuwa, vyombo hivyo vya habari vitoe elimu kwa Wananchi juu ya umuhimu wa kutoa taarifa sahihi wakati wa sensa, kwani utoaji wa taarifa sahihi ni jambo muhimu sana katika sensa, ambapo ikiwa taarifa zitakazokusanywa zitakuwa sahihi maana yake kutakuwa na Sera na Mipango sahihi ya maendeleo ya nchi kwa ujumla.
*“Serikali inapokuwa na takwimu sahihi itafanya maamuzi sahihi ambayo yataakisi hali iliyopo ya watu wake na mazingira wanayoishi,”* alifafanua Naibu Katibu Mkuu huyo.
Aidha, amevitaka vyombo hivyo vya habari kuwa na angalau na kipindi kimoja kwa wiki kinachozungumzia sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 pamoja na masuala muhimu yatakayomfanya mwananchi kujiamini na kushiriki vyema katika sensa hiyo.
Kwa upande wake, Kamisaa wa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022, Anne Makinda amevipongeza vyombo vya habari kwa namna vinavyoshiriki kutoa elimu ya sensa kwa Wananchi kupitia vipindi mbalimbali vya redio, televisheni, mitandao ya kijamii pamoja na habari na makala kupitia magazeti mbalimbali.
*“Sisi wenyewe tusingeweza kufika maeneo yote ya Tanzania, lakini kupitia vyombo vyenu vya habari mmeweza kuwafikia asilimia kubwa ya Watanzani, ambapo mmetoa elimu kwa makundi yote ya Watanzania, kama vile wakulima, wafugaji, vijana, wazee na watu wenye ulemavu”* alifafanua Makinda.
Naye Mhariri Mkuu wa EFM Redio na TV E, Scholastica Mazula ameiomba ofisi ya Takwimu kuandaa kikosi maalum chenye uelewa mkubwa wa masuala ya sensa na kupita katika vyombo vyote vya habari hapa nchini, kwa ajili ya kutoa elimu na manufaa ya sensa kwa Watanzania na Taifa kwa ujumla.