Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Pauline Gekul akiwa katika Picha ya pamoja na Miss Tanzania 2022 Halima Kopwe leo Mei 27, 2022 wakati Mlibwende huyo alipotembelea Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dodoma kuona Shughuli za Muhimili huo.
Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo (katikati) akiwa katika Picha ya pamoja na Mlibwende wa Tanzania kwa Mwaka 2022 ( Miss Tanzania 2022 ) Halima Kopwe na wenzie mshindi wa pili na watatu pamoja na Kamati ya Maandalizi ya shindano hilo mara baada ya kutembelea na kuona Shughuli za Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dodoma leo Mei 27, 2022 Dodoma.
……………………………………………
Na Shamimu Nyaki – WUSM, Dodoma
Naibu Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe.Pauline Gekul, ametoa wito kwa Mlibwende wa Tanzania mwaka 2022 Halima Kopwe Kuipeperusha na kuitangaza vyema Tanzania ndani na Ulimwenguni kupitia taji alilonalo.
Naibu Waziri ametoa rai hiyo leo Mei 27, 2022 Dodoma alipokutana na kufanya Mazungumzo na mrembo huyo, katika mualiko aliompatia wa kulitembelea Bunge la Tanzania, ili kuona shughuli za Bunge hilo.
“Wewe ndio umebeba jukumu la kuitangaza nchi yetu, umebeba Utamaduni wetu pamoja na lugha yetu adhimu ya kiswahili, tunaamini utatangaza vyema vivutio vya Tanzania popote utakapokua na utakua Balozi mzuri kwa nchi yetu” alisema Mhe.Gekul.
Mhe. Gekul pia alimtaka mrembo huyo kudumisha nidhamu, huku akiitaka Kamati ya Miss Tanzania kumlea vyema miss huyo ili tasnia ya urembo iendelee kuheshimiwa zaidi na ivutie vijana wengi ambao wanatamani kuingia hatimaye Tanzania iwe kinara katika nyanja hiyo.
Kwa upande wake Miss huyo Halima Kopwe ameishukuru Serikali kwa mchango mkubwa inayotoa katika kulea Sanaa na tasnia ya Urembo nchini, huku akiahidi Kuipeperusha vyema nchi katika kipindi chote atakachoshikilia taji hilo na baadae ambapo tayari ameingia kwenye rekodi za ulimbwende nchini.