****************
NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
WAKALA wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) imekusudia kufuta makampuni 5,676 ambapo kati ya hayo makampuni 5,284 ni yaliyosajiliwa hapa nchini na makampuni 392 ni ya yaliyosajiliwa nje ya nchi na kupata hati ya Utambuzi.
Ameyasema hayo leo Mei 27,2022 Kaimu Mkurugenzi Idala ya Makampuni na Majina ya Biashara Bw.aMeinrad Rwenyemamu wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Ofisi za BRELA Jijini Dar es Salaam.
Amesema wamekusudia kufuta makampuni hayo kwa kushindwa kukidhi takwa la kisheria la kuwasilisha taarifa za mwaka kwa kampuni zilizosajiliwa hapa nchini au mizani ya mwaka kwa kampuni zilizosajiliwa nje ya nchi kwa zaidi ya miaka 15.
“Endapo kampuni husika, wanahisa au wadeni wa kampuni ikiwemo taasisi za kifwdha na watumishi wa kampuni wanaamini kwamba kampuni iliyoko kwenye orodha hii inafanya biashara na kwamba inapaswa kubaki kwenye Daftari la Makampuni watoe taarifa kwa Msajili wa Makampuni”. Amesema
Aidha BRELA imetoa rai kwa makampuni yaliyosajiliwa chinibya sheria ya Makampuni, sura 212 ambayo hayakuorodheshwa kwenye Orodha ya awamu ya kwanza, kutekeleza matakwa ya sheria hiyo kwa kuwasilisha taarifa za mwaka ili kuepuka kufutwa kwenye Daftari la Makampuni kwani zoezi hili ni endelevu.