**********************
TAASISI ya ‘Dk Reginald Mengi Foundation’ (DRMF) kwa kushirikiana na Marafiki wa Dk Mengi wameandaa halfa maalumu itakayowakutanisha zaidi ya watu wenye ulemavu zaidi ya 1000 huku ikihudhuriwa viongozi wa Serikali, Mashirika Binafsi na Mabalozi mbalimbali.
Akizungumzia kuhusu hafla hiyo mbele ya waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Taasisi ya ‘Dk Reginald Mengi Foundation Shimimana Ntuyabaliwe alisema mgeni rasmi katika tukio hilo anatarajiwa kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Ajira,Vijana na Watu wenye Ulemavu Profesa Joyce Ndalichako.
Alisema halfa hiyo itakayohusisha matukio mbalimbali ikiwemo michezo, burudani, upimaji wa afya na kutoa shuhuda kuhusu Marehemu Dk Mengi inatarajiwa kufanyika Mei 29 katika Viwanja vya ‘Jakaya Kikwete Youth Park’ katikati ya Jiji la Dar es Salaam.
Alizitaja baadhi ya huduma za upimaji afya zitakazotolewa siku ya hafla hiyo kuwa ni pamoja na upimaji wa macho, kiwango cha sukari mwilini, tezi dume pamoja na kutoa ushauri wa kitabibu kwa wale watakaokuwa na changamoto mbalimbali.
“Pamoja na matukio hayo vilevile washiriki na wageni wote watapata fursa ya kula pamoja chakula cha mchana ikiwa ni ishara ya chakula alichokuwa akikiandaa Dk Mengi na kula na watu wenye ulemavu wapatao 5000 kila Mwaka kwa miongo mitatu” alisema Ntuyabaliwe
Alisema shughuli hiyo ni mahususi Kwa ajili ya kumbukizi ya moyo wake wa kujitolea na kujenga kizazi cha watanzania ambao watakumbuka na kujifunza historia yake na kujenga tabasamu kwa watanzania wenzao kitu ambacho marehemu Dk Mengi alikuwa akikifanya .
Alisema katika kipindi cha uhai wake Dk Mengi alijitolea na kufanya mambo mengi katika jamii ya watanzania Kwa kugusa maisha ya watu hususani watu wenye ulemavu na kuwapa matumaini wenzake ambao wengi walinufahika na uwepo wake.
“Kwa muktadha huu tunawasii watanzania wote kuendeleza mshumaa wa matumaini kwa kujenga moyo wa kujitolea kwa jamii kwani wahenga wana Usemi usemao kutoa ni moyo na siyo utajiri hivyo tunawahamasisha watanzania wote kwa umoja wao kujitolea kwa watu waliopo katika jamii zao” aliongeza Ntuyabaliwe