Waziri wa katiba na sheria ,Damas Ndumbaro akifunga semina ya siku tano kwa mawakili wa serikali iliyofanyika jijini Arusha.(Happy Lazaro)
Wakili Mkuu wa serikali , Gabriel Malata akizungumza wakati wa kufunga semina hiyo jijini Arusha leo.(Happy Lazaro)
************************
Happy Lazaro,Arusha.
Arusha.Waziri wa katiba na Sheria Dkt Damas Ndumbaro amewataka mawakili wa serikali hapa nchini kuzingatia maadili na weledi katika utendaji kazi na kujiepusha na vitendo vya rushwa ili kuisaidia serikali katika kusimamia maslahi ya umma.
Dkt Ndumbaro ametoa kauli hiyo leo jijini Arusha wakati akifunga mafunzo ya siku tano ya mawakili wa serikali iliyoandaliwa na ofisi ya wakili mkuu wa serikali nchini.
Amesema kuwa, kazi ya uwakili ni sekta nyeti inayoheshimika sana duniani ni lazima mawakili wajue wajibu wao kuwa wanaiwakilisha serikali katika mashauri mbalimbali ndani na nje ya nchi na kuwataka wakapambane na rushwa huku wao wakiepuka vitendo vya rushwa.
“Kesi ngingi mnazoendesha ni kubwa na zinaushawishi wa rushwa, epukeni kudai na kupokea rushwa ,tunajua vitendo vya rushwa vinafanyika kwa siri ila sisi tukiona mwenendo wako umebadilika ,Mavazi,unagari ya kifahari,nyumba nzuri lazima utaumbuka tu kuwa unajihusisha na rushwa tutakushughulikia”amesema.
Pamoja na kuwapongeza mawakili hao wa serikali kwa kuiwakilisha vema serikali na kufanikisha kuokoa kiasi cha zaidi ya sh,Trilioni 10 na mashamba 106 zilizotokana na madai mbalimbali na migogoro ya mikataba ndani na nje ya nchi,dokta Ndumbaro amewataka mawakili hao kutobweteka na sifa hizo badala yake kufanya kazi kwa ari zaidi na kwa kuzingatia misingi ya uwakili.
Amesema serikali itaendelea kutoa ushirikiano zaidi ili kuendelea kupewa mafunzo kama hayo ya mara kwa mara na kuwataka kuendelea kuishauri serikaki ili kuepusha kuingia kwenye migogoro isiyo na tija na kuisababishia hasara serikali.
Awali Wakili mkuu wa serikali ,Gabriel Malata aliishukuru serikali kwa kukubali kufanyika kwa mafunzo hayo ambayo yamekuwa na tija kwa washiriki wapatao 600 kutoka taasisi mbalimbali nchini .
Amesema kuwa,tangia kuanzishwa ofisi ya wakili mkuu wa serikali mwaka 2018 imekuwa ikitekeleza majukumu yake ya kuishauri serikali na kutatua migogoro mbalimbali inayohusu madai na usuluhishi , kufanya tafiti mbalimbali na kutambua mashauri yenye masilahi makubwa na madogo na kuishauri serikali namna ya kuyaendesha na kutunza kumbukumbu.
Amesema ofisi ya wakili mkuu wa serikali imekuwa ikishirikiana na mihimili mitatu ya serikali katika kuendesha mashauri yote yaliyopo mahakamani na ambayo hayajafunguliwa ili kuhakikisha mashauri hayo yanapungua au yanamalizika kwa usuluhishi kabla ya kufikishwa mahakamani.
“Pamoja na majukumu hayo ofisi ya wakili mkuu wa serikali imeweza kuiwakilisha vema serikali ndani na nje ya nchi kupitia mashauri ya madai na usuluhishi na kufanikiwa kuokoa takribani trilioni 10 na mashamba 106 yaliyokuwa yameporwa na watu wasiostahili tangu kuanzishwa kwa ofisi hii”amesema.
Aidha amesema kuwa,ofisi ya wakili mkuu wa serikali imejipanga kuchangia ukuaji wa uchumi wa Taifa kwa kuhamasisha wawekezaji kuja kuwekeza nchini kwa kuwapatia huduma nzuri katika mikataba yao ya uwekezaji na kuepusha mikataba isiyo na tija kwa taifa.