*************
Kamati ya Bunge ya Afya, Maendeleo na Huduma za Jamii,ya Bunge la Zambia wamevutiwa na hatua ya Bohari ya dawa (MSD) kuanza kuzalisha baadhi ya bidhaa za afya kwa kutumia wataalam wake wa ndani.
Hayo yamebainishwa hii leo, tarehe 26/5/2022 baada ya Kamati hiyo ya Afya kutoka Zambia, kuitembelea MSD kwa lengo la kujifunza na kubadilishana uzoefu katika masuala yanayohusu mnyororo wa ugavi wa bidhaa za afya.
Akizungumza kwaniaba ya ujumbe huo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo ya Bunge ya Afya, Maendeleo na Huduma za Jamii, ya Bunge la Zambia, Mhe.Dkt. Christopher K. Kalila amesema wamevutiwa na hatua ya Bohari ya dawa (MSD) kuanza kuzalisha baadhi ya bidhaa za afya kwa kutumia wataalam wake wa ndani.
Mhe.Dkt. Kalila ameongeza kuwa MSD Tanzania ni kama pacha wa Bohari ya Dawa ya nchini Zambia, kwani sheria yao pia imefanyiwa mabadiliko na kuiwezesha Bohari hiyo kuanza kuzalisha bidhaa za afya.
“Ni vyema taasisi zetu hizi mbili zikawa karibu ili kubadilishana uzoefu, na utaalamu katika maeneo mabalimbali ili kusukuma kwa pamoja ajenda ya uanzishaji wa viwanda vya bidhaa za afya na kuondoa utegemezi wa bidhaa kutoka nje sambamba na kupunza gharama.” Alisema
Dkt. Kalila
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa MSD Mavere Tukai amesema kwa pamoja na nchi nyingine kama Zambia yanaweza kufanyika mazungumzo ya pamoja ya kuwezesha ununuzi wa pamoja wa bidhaa za afya, kupitia mpango wa manunuzi ya pamoja ya SADC unaoratibiwa na MSD kwa nchi 16, kwa kupitia mpango huo, nchi wanachama zitanufaika, sambamba na kupaisha soko la viwanda vya ndani.
Wajumbe wa Kamati hiyo pamoja na mambo mengine wametembelea viwanda vya MSD vya kuzalisha barakoa, pamoja na kiwanda cha dawa cha Keko Pharmaceuticals, kinachosimamiwa na MSD.