*********************
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya katika kipindi cha kuanzia tarehe 22/05/2022 hadi tarehe 24/05/2022 limefanya misako na doria katika maeneo Mpakani Wilaya ya Mbarali, Mkola Wilaya ya Chunya na Mlima Nyoka Wilaya ya Mbeya na kufanikiwa kuwatia mbaroni wahamiaji haramu 63 wote wanaume raia wa nchini Ethiopia kwa kosa la kuingia nchini bila kuwa na kibali.
Katika mahojiano wameeleza kuwa wahamiaji hao walikuwa wakisafirishwa kuelekea nchini Malawi. Aidha katika misako hiyo wasafirishaji ambao ni watanzania wawili wamekamatwa ambao ni 1. KURWA NGORO [35] Dereva na Mkazi wa Makambako ambaye alikuwa akitumia gari yenye namba za usajili T.386 CWG aina ya Mitsubishi Dion na 2. PAUL NORBERT MWAMKONGA [47] Dereva, Mkazi wa Iringa ambaye alikuwa akitumia gari yenye namba za usajili T.139 BSE aina ya Toyota Super Custom Hiace.
Sambamba na hilo, Gari nne zilizokuwa zikitumika kuwasafirisha wahamiaji hao zimekamatwa ambazo ni:-
- 386 CWG aina ya Mitsubishi Dion rangi nyeupe.
- 139 BSE aina ya Toyota Super Custom Hiace.
- 309 ANX aina ya Mitsubishi Fuso.
- 423 BAK aina ya Toyota Mark II Grand.
Jeshi la Polisi Mkoani hapa linaendelea na msako wa mtandao wa watu wanaojihusisha na usafirishaji wa wahamiaji haramu hasa raia wa nchini Ethiopia na Somalia.
Aidha Jeshi la Polisi linatoa wito kwa wananchi kuacha kujihusisha na biashara haramu ya usafirishaji wa binadamu kwani ni kinyume cha sheria. Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linaendelea kuimarisha ulinzi na usalama katika maeneo yote ili kuzuia na kudhibiti uingizaji na upitishaji wa bidhaa za magendo na usafirishaji haramu wa binadamu.
Jeshi la Polisi linatoa rai kwa wananchi kujikita katika biashara halali vinginevyo watafirisika, watafungwa na vyombo vyao vya usafiri vitataifishwa na serikali kutokana na kuhusika katika usafirishaji haramu wa binadamu au uingizaji wa bidhaa za magendo.