Na Mwandishi wetu, Simanjiro
WANAWAKE wa Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara wamepatiwa elimu mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ujasiriamali kupitia Madiwani wa viti maalum na viongozi wa jumuiya ya Umoja wa wanawake (UWT) Simanjiro.
Mwenyekiti wa UWT wa Wilaya ya Simanjiro, Agness Brown Ole Suya amesema wamekutana na wanawake mbalimbali kwa kuwapa elimu ya ujasiriamali na kuwasihi wale waliochukua mikopo ya asilimia 4 ya wanawake kutoka Halmashauri warejeshe kwa wakati.
“Tunaporejesha mikopo hiyo ya asilimia nne kwa wakati inatupa uaminifu sisi wanawake lakini pia tunatoa fursa kwa wanawake wengine wapatiwe mikopo na kujiinua kiuchumi,” amesema.
Diwani wa Viti maalum Tarafa ya Naberera, Bahati Patson amesema wamepitia Kata ya Loiborsiret na kukutana na wanawake wanaofuga nyuki kupitia mizinga na kunufaika na asali.
Diwani wa Viti maalum Tarafa ya Emboreet, Namnyaki Edward amesema wanawake ni jeshi kubwa na wanasaidia familia ipige hatua hivyo wanapaswa kuungwa mkono.
Diwani wa viti maalum wa Tarafa ya Moipo, Paulina Makeseni amesema hivi sasa wanawake hawakai chini wamekuwa msaada mkubwa kiuchumi katika jamii ya wafugaji tofauti na awali.
Katibu wa UWT Wilaya ya Simanjiro, Leokadia Fisso amesema kwenye ziara hiyo pia wamesikiliza kero za wanawake na kuhamasisha wagombee nafasi mbali mbali ndani ya chama na jumuiya zake.
“Pia tumetembelea miradi mbalimbali inayotekelezwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye Wilaya ya Simanjiro,” amesema Fisoo.
Amesema wamehamasisha wanawake na wananchi kwa ujumla kujitokeza kuhesabiwa ifikapo Agosti 23 mwaka huu na kueleza umuhimu wa sensa.
Amesema wamehamasisha uundaji wa vikundi vya maendeleo kwa wanawake hao ili kujinyanyua kiuchumi.