Mkuu wa Wilaya ya Bahi Mhe.Mwanahamisi Munkunda akifungua mafunzo wilayani hapo kupitia Mradi wa Kudhibiti Sumukuvu Tanzania- TANIPAC kwa kutoa kipaumbele katika suala la kuelimisha jamii ya Wilaya ya Bahi juu ya usalama wa chakula hususan katika udhibiti wa sumukuvu ili kuweza kukabiliana na tatizo hilo.Mkuu wa Wilaya ya Kondoa Dkt. Hamisi Mkanachi akifungua mafunzo wilayani hapo kupitia Mradi wa Kudhibiti Sumukuvu Tanzania- TANIPAC kwa kutoa kipaumbele katika suala la kuelimisha jamii ya Wilaya ya Kondoa juu ya usalama wa chakula hususan katika udhibiti wa sumukuvu ili kuweza kukabiliana na tatizo hilo
*************************
SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) limeendelea na utoaji wa mafunzo kupitia Mradi wa Kudhibiti Sumukuvu Tanzania- TANIPAC kwa kutoa kipaumbele katika suala la kuelimisha jamii ya Wilaya ya Bahi na Kondoa juu ya usalama wa chakula hususan katika udhibiti wa sumukuvu ili kuweza kukabiliana na tatizo hilo.
Akizungumza wakati akifungua Mafunzo hayo wilayani Bahi Mkuu wa Wilaya ya Bahi Mhe.Mwanahamisi Munkunda ameipongeza TBS kwa kuhakikisha inatoa elimu kwa walengwa hususan kwenye sekta ya Kilimo ili kuona ni namna gani wanaweza kudhibiti sumukuvu kwenye mazao
“Ninapongeza sana jitihada za TBS kwa kupanga mafunzo haya yafanyike katika wilaya hii na mkakati mlionao wa kuendelea kuelimisha wananchi wa wilaya yetu ili waweze kukabiliana na uchafuzi wa sumukuvu katika mazao haya”. Amesema Mhe. Munkunda
Amesema Sumukuvu huathiri zaidi mazao ya mahindi na karanga ambayo ni sehemu muhimu ya chakula chetu hapa nchini. Kwa sababu hiyo tunapaswa kuzingatia mikakati ya kukabiliana na changamoto ya sumukuvu ili vyakula vyetu viendelee kuwa salama kwa muda wote.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kondoa Dkt. Hamisi Mkanachi wakati akifungua mafunzo hayo kwa upande wa Kondoa amesema mafunzo hayo kimsingi yana umuhimu wa pekee katika kuona kwamba bidhaa zitokanazo na mazao hayo, zinazalishwa kwa kufuata viwango, kanuni bora za usindikaji na kanuni bora za usafi.
“Kupitia Mafunzo haya tutakuwa tunazalisha bidhaa ambazo zinamhakikishia mlaji afya na usalama wake, lakini pia kwa upande wa pili kumuwezesha mzalishaji kufanya biashara ya chakula inayokubalika kwa wingi sokoni”. Amesema Mhe.Mkanachi.
Aidha amewasihi watalaamu wa afya, lishe, kilimo, mifugo, biashara na maendeleo ya jamii kutoka katika Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa kuendelea kutilia mkazo na kutoa kipaumbele katika kutekeleza mikakati ya kuimarisha usalama wa chakula ikiwa ni pamoja na kudhibiti uchafuzi wa sumukuvu.
Nae Meneja wa Tehama TBS, Bw.Jabir Abdi amesema Kiafya sumukuvu madhara yake ni udumavu na magonjwa kama kansa lakini kiuchumi tutashindwa kufanya biashara na nchi nyinginezo na TBS itaendelea kutoa elimu hii katika maeneo tofauti ili kuhakikisha Tanzania inadhibiti sumukuvu.