Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Pwani Christopher Myava Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake.
…………………………………………….
NA VICTOR MASANGU,PWANI
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoa wa Pwani imekemea vikali na kuwaonya baadhi ya makundi ya watu wanaojihusisha na kufanya utapeli wa kuuza ardhi kiholela na kusababisha kuibuka kwa migogoro.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Pwani Christopher Myava alipokuwa akitoa taarifa ya utendaji kazi ya robo ya tatu ya kuanzia mwezi januari mwaka huu.
Kamanda huyo alisema kuwa kuna baadhi ya watu wanatuhumiwa kuuza eneo kwa mtu zaidi ya mmoja jambo ambalo limekuwa chanzo cha kutoishq kwa migogoro ya ardhi katika mkoa huo.
Myava alisema Taasisi hiyo iko kazini kupambana na watu hao wanaodaiwa kushiriki kufanya utapeli ili wasiwaingize wawekezaji wenye lengo la kupata maeneo katika mkoa huo na kuzirotesha uwekezaji
Alisema kati ya malalamiko yaliyopokelewa katika kipindi hicho 17 yanahusiana na migogoro ya ardhi ambayo inadaiwa kuchangiwa na watu wanaodaiwa kuwa matapeli.
Alisema malalamiko 98 yalipokelewa katika kipindi cha miezi mitatu kati ya hayo 51yalihusu rushwa ambayo yalianzishiwa majalada ya uchunguzi huku malalamiko ya 47 yakielezwa kuwa hayakuhusu rushwa.
Mkuu huyo wa Takukuru pia amewatahadharisha wagombea wa nafasi mbalimbali kwenye uchaguzi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kijiepusha kujihusisha na vitendo vya rushwa.
“Nawaambia Takukuru hatujalala tuko kazini tutazuia vitendo vyote vyenye viashiria vya rushwa, na kwa matapeli wa ardhi tunaendelea kuchunguza malalamiko yaliyoletwa kukomesha tabia hii isituchafulie mkoa wetu” alisema .
Katika kipindi cha miezi mitatu TAKUKURU imeeleza kuwa imefuatilia miradi 182 katika sekta ya afya, Elimu, ujenzi na maji yenye thamani ya sh. Bilioni 8.4.
Kadhalika aliongeza kuwa lengo lao kubwa ni kuendelea kupambana usiku na mchana ili kuweza kuthibiti wimbi la vitendo rushwa na kuwataka wananchi kuwafichua wale wote ambao wanahujumu miradi ya maendeleo.