************************
Mbunge wa Jimbo la Ngara Mkoani Kagera,Mh. Ndaisaba George Ruhoro ameitaka Serikali kuitengeneza barabara ya Lusahunga hadi Rusumo kwa kiwango bora cha Lami ili kuchochea uchumi wa taifa kutokana na umuhimu wa barabara hiyo
Akichangia Hotuba ya Makadirio ya Bajeti ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, Bw Ruhoro amesema Barabara hiyo yenye urefu wa Kilomita 92 imekuwa ikitumika kusafirisha mizigo kutoka Bandari ya Dar es Salaam kwenda nchi jirani za Rwanda, Burundi na DRC na hivyo kuongeza pato la taifa.
Amesema kutokana na kutumiwa na magari mengi makubwa, barabara hiyo imekuwa ikiharibika mara kwa mara na wakati mwingine kusababisha ajali na uharibifu wa magari Bw Ruhoro pia ameitaka serikali kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Murugarama – Rulenge hadi Kumbuga wilayani Ngara ili ijengwe kwa kiwango cha Lami kurahisisha usafirishaji wa madini ya Nickel yanayotarajiwa kuongeza pato la taifa kwa kati ya Sh Trilioni 17 hadi Trilioni 20.