Naibu Waziri Wa Elimu Sayansi na Teknolojia Mhe.Omary Kipanga akipita katika baadhi ya mabanda ya wabunifu walioshiriki katika Ufunguzi rasmi wa Maadhimisho ya Saba ya Wiki ya Utafiti na Ubunifu yaliyofanyika leo Mei 24,2022 katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam .Naibu Waziri Wa Elimu Sayansi na Teknolojia Mhe.Omary Kipanga akizungumza katika Ufunguzi rasmi wa Maadhimisho ya Saba ya Wiki ya Utafiti na Ubunifu yaliyofanyika katika leo Mei 24,2022 Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Naibu Makamu Mkuu wa Chuo-UTAFITI Prof.Bernadeta Kilian akizungumza katika Ufunguzi rasmi wa Maadhimisho ya Saba ya Wiki ya Utafiti na Ubunifu yaliyofanyika katika leo Mei 24,2022 Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Makamu Mkuu wa Chuo cha Dar es Salaam, Prof.William Anangisye akizungumza katika Ufunguzi rasmi wa Maadhimisho ya Saba ya Wiki ya Utafiti na Ubunifu yaliyofanyika katika leo Mei 24,2022 Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
Baadhi wadau wa utafiti na ubunifu wakifuatilia Ufunguzi rasmi wa Maadhimisho ya Saba ya Wiki ya Utafiti na Ubunifu yaliyofanyika katika leo Mei 24,2022 Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
(PICHA ZOTE NA EMMANUEL MBATILO)
************************
NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
Serikali imefadhili jumla ya miradi 242 ya sayansi, teknolojia na ubunifu katika sekta mbalimbali ikiwemo kilimo na mifugo, afya, nishati, maliasili, na viwanda yenye thamani ya jumla ya shilingi bilioni 51.6.
Kati ya miradi 150 ni ya utafiti, 60 ni ya ubunifu na 32 ni ya kuboresha miundombinu ya maabara za utafiti katika Taasisi za Elimu ya Juu na Utafiti na Maendeleo.
Ameyasema hayo leo Mei 24,2022, Naibu Waziri Wa Elimu Sayansi na Teknolojia Mhe.Omary Kipanga wakati wa Ufunguzi rasmi wa Maadhimisho ya Saba ya Wiki ya Utafiti na Ubunifu yaliyofanyika katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
Amesema Serikali kupitia MTUSATE, imewajengea uwezo watafiti 579 kwa ufadhili katika masomo ya ngazi ya uzamili na uzamivu.
Aidha amesema Serikali imefadhili mradi wa Vituo vya Umahiri Kusini Mashariki mwa Afrika (Eastern and Southern Afrika HigherEducation Centres of Excellence – ACE-II), ambao pamoja na mambo mengine mradi unalenga kujenga uwezo wa Taasisi za Elimu ya Juu kufanya tafiti zinazolenga kutatua changamoto katika jamii.
“Kupitia mradi huu imetoa Dola za Marekani milioni 24 ambazo ni mkopo kutoka benki ya dunia na tumesomesha jumla ya wataalam 799 (264 uzamivu (PhD) na 535 umahiri)”. Amesema Mhe.Kipanga.
Serikali imeongeza bajeti ya mikopo ya wanafunzi wa Elimu ya Juu kutoka shilingi bilioni 464 mwaka 2020/2021 hadi shilingi bilioni 570 mwaka 2021/2022 na hivyo kuongeza idadi ya wanafunzi wa mwaka wa kwanza wanaopata mikopo kutoka 55,000 hadi 76,000 na kufanya jumla ya wanufaika wa mikopo kwa mwaka kuongezeka kutoka 140,000 hadi wanafunzi 170,000.
“Katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, imewaibua na kuwatambua jumla ya wabunifu na wavumbuzi wachanga 1,785, kati yao, 200 wanaendelezwa na Serikali ili bunifu zao zifikie hatua ya kuwa bidhaa na kutumika kutatua changamoto mbalimbali katika jamii”. Amesema
Amesema Serikali inatambua mchango wa utafiti na ubunifu kama nyenzo muhimu katika kuboresha na kurahisisha maisha yetu kwa kuokoa muda katika utendaji kazi, kuongeza tija na ubora katika uzalishaji wa bidhaa na hata utoaji huduma.
Utafiti na ubunifu, na maendeleo endelevu ya kijamii na kiuchumi vinakwenda sambamba. Kwa mantiki hiyo ni lazima watafiti, wabunifu na wavumbuzi katika sekta zote wachukue hatua za makusudi kubuni na kuzalisha teknolojia kwa ajili ya kuleta maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini.
“Wakati tukifanya hayo yote, ni muhimu pia kutafakari na kujiuliza ni kwa namna gani tunajitayarisha ili kunufaika kikamilifu na fursa zinazotokana na mabadiliko ya kiteknolojia yanayoendelea duniani kote”. Amesema Mhe.Kipanga
Amesema matumizi ya teknolojia zinazoambatana Mapinduzi ya Nne ya Viwanda, yamedhihirika katika sekta za fedha, elimu, usafirishaji, kilimo, viwanda na huduma za afya.
Aidha amesema jambo la msingi kwetu sisi kama nchi ni kuendelea kufanya utafiti na kubuni namna nzuri ambayo teknolojia na bunifu hizo zinavyoweza kutumika kwa manufaa ya maendeleo ya kiuchumi na ustawi wa jamii.
“Watafiti, wabunifu na wavumbuzi katika sekta zote, lazima wachukue hatua za makusudi kubuni na kutumia teknolojia zinazoibukia kwa ajili ya kuleta maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika nchi yetu”. Amesema
Pamoja na hayo amesema Serikali kupitia Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) imeandaa vipaumbele vya utafiti vya mwaka 2021/22 -2025/26 ambavyo vinavyoweka dira na mwelekeo wa utafiti, uvumbuzi na ubunifu wa teknolojia kwa kuzingatia Mipango ya Maendeleo ya nchi yetu.
Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo cha Dar es Salaam, Prof.William Anangisye amesema kuwa kwa kutambua umuhimu wa tafiti na ubunifu katika kutatua changamoto zinazoikabili jamii ya Watanzania na Taifa kwa ujumla, Chuo hicho kimekuwa kikitenga bajeti kwa kutegemea vyanzo vya ndani ambapo kwa mwaka wa fedha 2018/2019 Chuo kilitenga Shilingi Bilioni 1.0 kwa ajili ya utafiti na ubunifu.
“Idadi ya fedha za utafiti na ubunifu iliongezeka hadi Shilingi Bilioni 1.4 mwaka 2019/2020; Shilingi Bilioni 1.9 mwaka 2020/2021; na Shilingi Bilioni 3.15 kwa mwaka wa fedha 2021/2022”. Amesema
Amesema Wiki ya Utafiti na Ubunifu, mbali na mambo mengine, inalenga kuweka bayana matokeo ya tafiti na kuwajulisha wadau na umma kwa ujumla kuhusu shughuli za utafiti na ubunifu zinazofanywa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.