Maafisa wa TBS wakitoa elimu ya viwango ikiwa ni pamoja na namna ya kutuma maoni/malalamiko pale wanapokutana na changamoto zozote kwenye bidhaa katika soko la Ifunda wilayani Iringa.
Wanafunzi wa shule za Sekondari ya Lipuli na Lyandembela katika halmashauri ya wilaya ya Iringa wakijibu maswali baada ya kuelimishwa masuala ya viwango. TBS inato elimu kwa wanafunzi kujenga tamaduni ya masuala ya ubora kuanzia ngazi ya chini ili kuhakikisha bidhaa hafifu zinapungua sokoni.
***********************
Na Mwandishi Wetu
WANANCHI zaidi ya 15,000 katika Wilaya za Songwe, Njombe, Mufindi na Halmashauri ya Wilaya ya Iringa wamepatia elimu kuhusiana na umuhimu wa kununua bidhaa zilizothibitishwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) sambamba na kuhamasisha wafanyabiashara kusajili maduka ya chakula na vipodozi.
Kampeni hiyo ya kutoa elimu kwa wanachi hao ilianza tarehe 07.05.2022 katika wilaya hizo na kuhitimishwa mwanzoni mwa wiki hii ambapo ilifanyika katika maeneo mbalimbali yakihusisha na shule za msingi na sekondari, masoko, stendi, minadani na maeneo mengine ya wazi ambapo wananchi walijitokeza kwa wingi kupata elimu na ufahamu wa masuala mbalimbali yahusuyo ubora wa bidhaa.
Akizungumzia kampeni hiyo Mkuu wa Idara ya Elimu Sekondari wa Halmashauri ya Mji wa Mafinga, Stephen Shemdoe, aliipongeza TBS kwa kutoa elimu kwa wanafunzi na alishauri kuanzishwa kwa klabu za kudumu za masuala ya viwango katika shule za sekondari kwa miaka ijayo ili elimu hiyo iwe endelevu.
Kwa upande wake Meneja Uhusiano na Masoko wa TBS, Gladness Kaseka aliwakumbusha wananchi kutambua kuwa vita ya bidhaa hafifu sio ya TBS pekee, bali ni ya Taifa kwa ujumla.
“Katika kampeni hii tumeweza kuwafikia wananchi 15,865 kati yao wanafunzi wa shule za msingi na sekondari 9,144 na wananchi 6,721,” Alisema Kaseka.
Kaseka aliwafafanulia wanafunzi pamoja na walimu kuhusu umuhimu wa viwango katika maisha yao ya kila siku vile vile kuwafahamisha fursa ya huduma bure kwa wajasiriamali wadogo.
Aliwataka wananchi waliopata elimu hiyo kuhakikisha wanakuwa mabalozi kwa kuhamasisha ubora katika jamii wanazoishi.
Aidha, alitoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa taarifa pindi wanapokutana na bidhaa zilizokwisha muda wake au wanapotilia shaka bidhaa yoyote katika soko.
Kwa upande wa wafanyabiashara aliwataka kuhakikisha wanafuatilia taratibu sahihi za usajili wa bidhaa au majengo ya chakula na vipodozi kwa kutembelea ofisi ya TBS iliyopo karibu au kupiga katika kituo cha huduma kupitia mawasiliano yaliyotolewa.
Kampeni ya kuelimisha umma inayotolewa na shirika hiyo ni endelevu itaendelea katika wilaya za mikoa ya Kaskazini.