Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye, akizungumza wakati wa kikao na Wakandarasi kuhusu ujenzi wa Km 4,442 za Mkongo wa Taifa kilichofanyika leo Mei 23, 2022,jijini Dodoma.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Jim Yonazi akizungumza wakati wa kikao na Wakandarasi kuhusu ujenzi wa Km 4,442 za Mkongo wa Taifa kilichofanyika leo Mei 23, 2022,jijini Dodoma.
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye (Mb) akimkabidhi cheti cha cha kukamilisha ujenzi wa kilomita 72 za Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano na kuunganisha Ofisi za Serikali zilizopo eneo la Mtumba jijini Dodoma kwa Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, Mhandisi Petter Ulanga katika kikao kazi na Wakandarasi kuhusu ujenzi wa Km 4,442 za Mkongo wa Taifa kilichofanyika leo Mei 23, jijini Dodoma
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye(Mb) akimkabidhi cheti na nyaraka za michoro Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, Mhandisi Peter Ulanga inayoonyesha jinsi na namna miundombinu ya Mkongo wa Taifa ulivyojengwa kutoka Mangaka-Mtambaswala (kilomita 72) na Arusha-Namanga (kilomita 105) ili kuliwezesha shirika kusimamia na kuendesha Mkongo huo
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye (Mb) akimkabidhi cheti cha mradi wa Mkongo wa Taifa uliokamilika mwaka 2021/2022 Mkurugenzi Mtendaji wa Kandarasi ya Raddy Fibre Solution Ltd, Ramadhani Mlanzi katika kikao kazi na Wakandarasi kuhusu ujenzi wa Km 4,442 za Mkongo wa Taifa kilichofanyika leo Mei 23, jijini Dodoma.
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye (Mb) wakifurahi na kupongezana na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Jim Yonazi mara baada kikao kazi na Wakandarasi kuhusu ujenzi wa Km 4,442 za Mkongo wa Taifa kilichofanyika leo Mei 23, jijini Dodoma.
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye (wa katikati aliyeketi) akiwa katika picha ya Pamoja na Wakandarasi wa Mkongo wa Taifa uliokamilika mwaka 2021/2022 mara baada ya Waziri Nape kuzungumza na Wakandarasi hao kwenye kikao kazi na Wakandarasi kuhusu ujenzi wa Km 4,442 za Mkongo wa Taifa kilichofanyika leo Mei 23, jijini Dodoma.
………………………………………….
Na Alex Sonna-DODOMA
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye amesema kuwa kwasasa serikali ipo kwenye mchakato wa kuhamishia shughuli zote za mkongo wa Taifa kwenye Shirika la Mawasiliano Tanzania(TTCL).
Hayo ameyasema leo Mei 23,2022 jijini Dodoma wakati wa kikao kazi na wakandarasi wajenzi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano
“Kama nilivyozungumza Bungeni wakati wa wasilisho la hotuba ya Bajeti ya Wizara hii Mei 20, 2022 kuwa tupo katika mchakato wa kuhamishia shughuli zote za Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano kwa Shirika letu la TTCL, Wizara imeulea mpaka umekuwa na sasa upo tayari kukabidhiwa kwa Shirika hilo”, amesema
Hivyo sina mashaka na uwezo wa Mkurugenzi wa Shirika la TTCL katika kusimamia shughuli zote za Mkongo na ana matumaini makubwa kuwa ataweza kubeba jukumu hilo pindi mchakato wa utakapokamilika kuukabidhi kwa Shirika hilo utakapokamilika
Waziri Nape ameagiza ujenzi wa mkongo wa taifa ufanyike kwa ubora huku akionya mkandarasi yeyote atakayebainika kufanya vibaya atakuwa amejifungia kufanya kazi na Wizara na serikali nzima.
“Mimi siamini katika kumpiga mtu buti kabla ya kumwambia, mwambie kwanza, sasa imebidi niyaseme haya vizuri tumeweka fedha ya umma kwenye hii miradi lazima ifanyike kwa ubora na kwa wakati, kazi hii ya mbele ni kubwa zaidi na fursa zipo ila zitapimwa kwa kazi uliyopewa nyuma…Niwahakikishie mkifanya kazi vizuri mtafurahia kufanya kazi na sisi lakini mkifanya vibaya mtajutia kufanya kazi na sisi.”amesema Waziri Nape
Aidha Waziri Nape amesema kwa Mwaka 2022/23 serikali inatarajia kujenga zaidi ya kilomita 1600 na vituo vipya 15 na lengo ni kufika Wilaya 81 na urefu wa kilomita 14,361 sawa na asilimia 95 ya lengo kubwa la kufikia kilomita 15,000 ifikapo Mwaka 2025.
Amesema kuwa tangu kuanza kujengwa kwa Mkongo huo mwaka 2009, ujenzi wake umefikia kilomita 8,319 na zaidi ya Sh.Bilioni 670 zimetumika na una vituo kwenye mikoa 25 Tanzania bara na Wilaya 43 kati ya 139 sawa na asilimia 30.9 zimefikiwa na kwamba bado kuna kazi kubwa ya kufanya.
“Mwaka 2021/22 zilitengwa Sh.Bilioni 170 kwa ajili ya kujenga kilomita 4,442 na kuongeza uwezo kutoka 200G kwenda 800G, jumla ya mikataba 22 ilisainiwa na ilihusisha kampuni nane, takwimu zinaonesha kati ya kampuni hizo sita ni za watanzania kazi hii inapaswa kuisha Desemba 2022, ikikamilika yote tutakuwa tumefikia kilomita 12, 761 kati ya 15,000 za lengo la Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2025,”amesema
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dk.Jim Yonaz, amesema lengo la ujenzi wa mkongo huo ni kufikia kilomita 15,000 ifikapo Mwaka 2025 na unaoongoza Afrika Mashariki na Kati.
Awali akitoa taarifa ya mradi wa mkongo wa taifa, Mkurugenzi wa TEHAMA wa Wizara hiyo, ,Mlembwa Mnako amesema mkongo huo umesaidia kupunguza gharama za kusafirisha mawasiliano kwa njia ndefu ambapo awali walikuwa wakitumia satelaiti.