Na Abby Nkungu, Singida
MKUU wa Mkoa wa Singida Dk. Binilith Mahenge amewaagiza Wakuu wa
wilaya, Wakurugenzi wa halmashauri za wilaya na Manispaa mkoani humo
kuhakikisha wanafikia malengo waliojiwekea kwa kuwapatia chanjo ya polio
watoto wote walio chini ya umri wa miaka mitano.
Akiongoza Uzinduzi wa kampeni ya siku nne ya chanjo ya matone ya
polio uliofanyika kimkoa katika Kata ya Iguguno wilayani Mkalama, Dk
Mahenge alisema iwapo malengo yatafikiwa, mkoa utakuwa na uhakika kuwa
unalea Taifa ambalo litaingia kwenye shughuli za uzalishaji likiwa na afya
njema.
Aidha, aliezea kazi kubwa iliyofanywa na Serikali ya Rais Samia
Suluhu Hassan kwa kutenga bajeti kubwa kwa Sekta ya afya ambapo Mkoa wa Singida
ulipokea zaidi ya Sh bilioni 30 kwa mwaka huu huku hospitali za wilaya zikijengwa
Ikungi, Manyoni, Mkalama na Halmashauri ya wilaya Singida pamoja na vituo
vya afya 15 katika wilaya zote.
“Nimeyasema haya ili kuonesha jinsi Rais wetu anavyotujali
Watanzania na ndio maana leo tupo hapa tunazindua kampeni hii ya polio baada ya
Serikali kutuwezesha” alisema Dk.Mahenge.
Awali, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dk Victorina Ludovick
alisema kuwa mkoa unatarajia kufikia jumla ya watoto 286,736 walio chini
ya miaka mitano kwa kipindi cha siku tatu na kwamba lengo ni kufika kwenye
maeneo yote ambapo itafanyika nyumba kwa nyumba .
Alitaja madhara ya ugonjwa wa Polio kuwa ni ulemavu wa ghafla wa
viungo na usiotibika kwa hiyo ni muhimu kwa kila mzazi na mlezi kuwatoa watoto
wao wenye umri tajwa ili wapate chanjo hiyo salama.
Dk.Ritha Willilo kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO) alitoa
mwito kwa wazazi kutoa ushirikiano wa hali ya juu kwa watoa huduma ya chanjo
hiyo ili malengo ya Serikali yaweze kutimia.
Baadhi ya wananchi waliohojiwa waliahidi kujitokeza kwa wingi
kuwapeleka watoto wao kwenye chanjo kwa kuwa sasa wameelimika vya kutosha na
kwamba wameachana na imani potofu zilizokuwa zikiwazuia kukubali chanjo
mbalimbali.
Kwa mujibu wa Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na
Maendeleo ya Awali ya Mtoto (PJT-MMMAM) 2021/22 – 2025/26, Serikali ya Tanzania
kupitia Sera ya Afya 2007 imewekeza sana katika kuboresha uhai wa mtoto kupitia
utoaji wa huduma bure za afya kwa akinamama wajawazito na watoto chini ya miaka
mitano.