***********************
Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) imeunga mkono na kuridhia hatua ya Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ndugu Samia Suluhu Hassan ya kuendeleza majadiliano na vyama vya siasa yenye lengo la kuimarisha demokrasia kupitia maridhiano ya kisiasa kwa maslahi ya taifa.
Aidha, CCM imesisitiza kuendeleza majadiliano hayo kwa dhumuni la kujenga jamii yenye usawa, uhuru wa kujieleza na kushiriki shughuli za kisiasa kwa kuzingatia maadili na sheria za nchi.
Akizungumza leo na waandishi wa habari, Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka, alisema Kamati Kuu ya CCM iliyoketi juzi, ilikutana kwa ajili ya kupokea kisha kujadili masuala mbalimbali ya kitaifa.
“Kamati kuu ilipokea na kujadili masuala ya mbalimbali ya kitaifa ikiwemo hatua zinazochukuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan katika kujenga maridhiano ya kisiasa nchini,”
Aliongeza kuwa: “Kamati Kuu imempongeza na kumuunga mkono Rais Samia kwa hatua anazoendelea kuchukua ikiwemo kukutana na kufanya mazungumzo na makundi ya kijamii katika kujenga amani, haki na maridhiano.”
Shaka alisema Kamati Kuu ya CCM imetambua na kuridhia dhamira ya dhati ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kufanya maridhiano kwa kuzingatia uendelezaji wa urithi, tunu na msingi imara wa ujenzi wa taifa ili kuviwezesha vizazi vijavyo virithi taifa jema na lililo imara.
Katibu huyo wa NEC Itikadi na Uenezi, alisema Chama kinatambua mazingira na mahitaji ya kisiasa yaliyopo ndani ya jamii, hivyo kufanikiwa kwa majadiliano hayo kutawanufaisha wananchi katika kuimarisha misingi ya utawala bora na utoaji huduma za kijamii.
“CCM ndicho chama kiongozi na kikomavu katika siasa za nchi yetu, kipo tayari kuendeleza mjadala wenye lengo la kuimarisha demokrasia endelevu kwa maslahi ya taifa,” alisisitiza.
Shaka alitoa rai kwa Watanzania kuendelea kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan kwani amekuwa kiongozi mwenye kuliunganisha taifa.