Na Lucas Raphael,Tabora
WAKALA wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijiini (RUWASA) Mkoani Tabora wamesaini mikataba 6 yenye thamani ya sh bil 3.4 kwa ajili ya kutekeleza miradi 6 ya maji katika wilaya 5 za Mkoa huo.
Akitoa taarifa ya miradi hiyo katika hafla ya utiaji saini jana, Meneja wa RUWASA Mkoani hapa Mhandisi Hatari Kapufi alisema miradi hiyo itatekelezwa katika wilaya za Uyui, Kaliua, Igunga, Nzega na Sikonge.
Alitaja vijiji vitakavyonufaika na miradi hiyo kuwa ni Songambele-Miyenze (Uyui), Kongo na Uhuru-mbiti (Uyui), Mwasung’o – Mwamapuli (Igunga), Igigwa-Wankolongo (Sikonge) na Usimba (Kaliua).
Vijiji vingine ni Muhugi, Ishiki, Mwantundu,Kasanga, Seki, Mwakabasa,Idilima na Ibushi wilayani Nzega ambavyo vitanufaika na miradi ya visima virefu 8 vitakavyochimbwa katika maeneo hayo.
Alibainisha kuwa serikali ina dhamira ya dhati kumaliza kero ya maji katika vijiji vyote vya Mkoa huo ili kumtua mama ndoo kichwani na kuongeza kuwa mwaka jana mikataba mingine 15 yenye thamani ya sh bil 16 ilisainiwa na utekelezaji unaendelea.
Mhandisi Kapufi alisisitiza kuwa timu yake imejipanga vizuri kusimamia miradi hiyo ili iwanufaishe wananchi na kuongeza kuwa kila Mkandarasi anatakiwa kuzingatia makubaliano yaliyoainishwa kwenye mkataba wake na si vinginevyo.
Akitoa nasaha zake kwenye hafla hiyo Mkuu wa Mkoa huo Balozi Dkt Batilda Burian aliishukuru serikali kwa kutoa kiasi hicho cha fedha ili kutatua kero ya maji katika vijiji vya Mkoa huo ambavyo havina huduma ya maji safi na salama.
Alisisitiza kuwa miradi hiyo ni muhimu sana kwa wananchi hivyo akaagiza Wakandarasi waliopewa kazi hizo kumaliza kwa wakati na katika kiwango kinachokubalika kama mikataba yao inavyoelekeza.
RC Batilda alibainisha kuwa hali ya upatikanaji maji kwa wakazi wa vijijini katika Mkoa huo kwa sasa ni asilimia 62 hivyo akasisitiza miradi yote inayotekelezwa katika maeneo mbalimbali Mkoani humo kukamilika haraka.
Alionya Wakandarasi wanaosua sua kutekeleza miradi wanayopewa na kuongeza kuwa hawatapewa kazi nyingine tena, huku akiwataka Wakuu wa Wilaya kufuatilia miradi inayotekelezwa katika maeneo yao ili ikamilike haraka.
Naye Katibu Tawala wa koa huo Msalika Makungu alisema miradi hiyo ni utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) hivyo akawataka Wakandarasi kufanya kazi hiyo kwa weledi mkubwa.
Wakuu wa wilaya Kisare Makori (Uyui), Dkt Yahaya Nawanda (Tabora), Peter Bura (Urambo) , Paul Chacha (Kaliua), ACP Divela Bulimba (Nzega) na John Pallingo (Sikonge) waliahidi kufuatilia miradi hiyo ili ikamilike kwa wakati.
Mwakilishi wa Wakandarasi hao Geofrey Oyaro aliishukuru serikali kupitia RUWASA kwa kuwaamini na kuwapatia kazi hizo na kumhakikishia Mkuu wa Mkoa kuwa watafanya kazi hiyo kwa weledi mkubwa na kwa wakati.
Mwisho.
Pichani…Mkuu wa Mkoa wa Tabora Balozi Batilda Burian (aliyeketi mstari wa mbele mwenye kitambaa) akiwa katika picha ya pamoja na Wakadarasi watakaoteleza miradi 6 ya maji katika wilaya 5 za Mkoa huo baada ya kusaini mikataba ili kuanza kazi hiyo.