**************************
Serikali ya Ujerumani imeahidi kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kutekeleza mradi wa utunzaji wa rasilimali za maji katika bonde la mto Katuma ambao utagharimu Euro Milioni nne, ambazo ni takribani shilingi za Tanzania Bilioni Kumi.
Ahadi hiyo imetolewa na Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Ushirikiano Ubalozi wa Ujerumani Dkt. Katrin Bornemann baada ya mazungumzo yaliyofanyika Jijini Dodoma na Katibu Mkuu Wizara ya Maji Mhandisi Anthony Sanga.
Amesema wataendelea na utekelezaji wa miradi katika majiji ya Mwanza na Tanga shughuli ambayo imekuwa ikifanywa kupitia Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ) na Benki ya Maendeleo ya Ujerumani (KfW).
Dkt. Bornemann amesema serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan imeonesha nia ya dhati ya kujenga mahusiano ambayo yamekuwepo kwa muda mrefu kati ya serikali ya Ujerumani na Tanzania.
“Tumekuja hapa leo ili kufikia makubaliano ya pamoja na uongozi wa Wizara ya Maji ili tushiriki katika kuondoa changamoto mbalimbali katika Sekta ya Maji. Nimekuwepo Tanzania kwa muda sasa. Nimekuwepo siku ya kilele cha Siku ya Maji Duniani iliyofanyika jijini Dar es Salaam. Niliwasikiliza viongozi wa Wizara ya Maji akiwemo Mheshimiwa Rais Samia. Serikali ya Ujerumani imeiona nia ya dhati ya serikali ya Tanzania kuendeleza mahusiano mema. Tuko tayari kushirikiana kuhakikisha changamoto za sekta ya maji zinapatiwa ufumbuzi.” Dkt. Bornemann amesema.
Kupitia kikao hicho, Katibu Mkuu Wizara ya Maji Mhandisi Anthony Sanga ameishukuru serikali ya Ujerumani kwa nia yake ya kuhakikisha changamoto kuhusu maji zinapata majibu.
Amesema maeneo mbalimbali ikiwemo hifadhi ya Taifa ya Katavi imekuwa ikikumbwa na ukame kutokana na changamoto mbalimbali ikiwemo shughuli za kibinadamu.
“Jambo hili limekuja katika muda muafaka na litasaidia kwa kiasi kikubwa kuhakikisha rasilimali za maji zinaendelea kutunzwa na kuhifadhiwa kwa ajili ya matumizi ya binadamu, Wanyama na kulinda mazingira.” Mhandisi Sanga amesema.