Naibu Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Kinondoni Bi. Elezabeth Mokiwa akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam kuhusu taarifa utekelezaji wa majukumu kwa kipindi cha miezi mitatu kuanzia January hadi March 2022.
*************
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM.
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Kinondoni imewasihi wananchi wa Kinondoni na Ubungo kutumia vizuri siku za kusikiliza Malalamiko na Kero zilizotengwa na taasisi hiyo lengo likiwa ni kuhakikisha vitendo vya rushwa vinatokemezwa.
Akizumgumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam kuhusu utekelezaji wa majukumu yake kwa kipindi cha miezi mitatu kuanzia January hadi March 2022, Naibu Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Kinondoni Bi. Elezabeth Mokiwa, amesema kuwa ofisi za TAKUKURU Mkoa na Wilaya ya ubungo kila siku ya Alhamisi ya mwisho wa mwezi wanasikiliza kero za wananchi.
Bi. Makiwa ameeleza kuwa katika kipindi hicho cha miezi mitatu wamepokea jumla ya taarifa 161 kati ya hizo, taarifa 81 zinazohusiana na vitendo vya rushwa.
Bi. Mokiwa amesema kuwa pia wamefungua majalada ya uchunguzi ambapo majalada 11 yapo katika hatua ya uchunguzi wa kina, jalada moja la uchunguzi wake umekamilika lipo kwa ofisi ya Taifa ya Mashtaka, 69 yaliobaki uchunguzi wake bado unaendelea.
“Tumefungua kesi mpya moja katika mahakama ya Wilaya ya Kinondoni na kufanya jumla ya kesi zinazoendelea mahakamani kuwa 12, huku kesi moja imetolewa hukumu na Jamhuri imeshinda” amesema Bi. Mokiwa.
Amefafanua kuwa wamefatilia miradi mbalimbali ya barabara yenye thamani ya sh. 11,229,118, 775.25 lengo ni kuhakikisha fedha zinatumika kwa usahihi kama ilivyoelekezwa na kuzingatia ubora, thamani ya fedha na muda husika.
Amesema kuwa wameendelea na utekelezaji wa mipango ikiwemo kuelimisha wananchi katika nyanja mbalimbali ili kuhakikisha malengo tarajiwa yanafikiwa na watu.
Bi. Mokiwa amesema katika kufanikisha mikakati yake wamejipanga kushirikiana na Chama cha Skauti chini ya Mpango wa TAKUSKA kwa kutoa elimu ya mapambano dhidi ya rushwa ikiwemo umuhimu wa ufuatiliaji wa Miradi ya Maendeleo.