Mkurugenzi wa Taasisi ya Mwanamke Initiatives Foundation, Fatma Mwasa akikabidhi msaada wa vifaa vya shule na mahitaji ya kila siku kwa Mkuu wa Chuo cha maendeleo ya wananchi Kilwa Masoko, Elabry Miombe.
*******************
Mwandishi wetu
Lindi. Taasisi ya Mwanamke Initiatives Foundation, imetoa msaada wa sh11 millioni kwa wanafunzi wasichana waliokosa fursa ya kumaliza masomo ya sekondari kwa sababu mbali mbali ikiwemo mimba waliopo katika vyuo vya maendeleo ya Jamii nchini.
Mkurugenzi wa Taasisi hiyo, Fatma Mwasa ametoa msaada huo leo ambao ni vifaa vya shule, sabuni za kuogea, kufulia, na nguo kwa wanafunzi 30 wanaotokea Zanzibar waliopo katika vyuo vya maendeleo ya jamii vya Kilwa Masoko na Kisarawe na wengine wa Bara.
kuwa Taasisi yake vile vile imetoa taulo za kike kwa ufadhili wa HQ ili kuwasaidia kuwa huru kendelea na masomo na michezo hata wanapokua katika ada zao za mwezi.
Amesema Taasisi ya Mwanamke initiatives Foundation ambayo inajishughulisha na masuala ya kuimarisha elimu ya kawaida na mafunzo ya amali zaidi visiwani Zanzibar kwa kushirikiana na wizara ya elimu visiwani humo imeona fursa ya kuwasaidia wanafunzi hao waliopo katika vyuo vya maendeleo ya jamii Tanzania bara iliyotangazwa na Rais Samiah Suluhu Hassan.
“Kama Watanzania tuna kila sababu ya kuitumia fursa hii kwa hiyo tumewaleta vijana kutoka Zanzibar wamekuja kusoma fani mbali mbali za umeme wa majumbani, ushonaji na fani ya ufundi” amesema Fatma Mwasa.
Ameongeza kuwa lengo lao kubwa ni wanafunzi hao waliokosa fursa ya kumaliza masomo ya sekondari waweze kupata vyeti vya kidato cha nne lakini pia wapate ujuzi ambao utawawezesha kujiajiri.
Fatma Mwasa amesema mwisho kabisa wa jambo hilo ni kuona wameweza kutengeneza ajira kwa vijana wote ambao wamewawezesha kuja kuoata mafunzo katika vyuo vya maendeleo ya wananchi vilivyopo Tanzania Bara.
Mkurugenzi wa Shirika lisilo la Kiserikali la Karibu Tanzania Organization, (KTO), Maggid Mjengwa amesema kuwa jumla ya wanafunzi 2600 walikosa fursa ya kumaliza masomo ya sekondari wamejiunga katika vyuo 54 vya maendeleo ya wananchi vilivyopo Tanzania bara kwa mwaka huu kwa mafunzo hayo ya miaka miwili.
Amesema taasisi yake ambayo inafanya kazi na vyuo vya maendeleo ya wananchi nchini ambavyo viko chini ya wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ina programu tatu ambazo ni elimu haina mwisho, mpira fursa na elimu ya makuzi na malezi kwa watoto.
Maggid amesema kuwa chuo cha maendeleo ya wanachi cha Kilwa Masoko ni moja wapo ya vyuo vilivyopokea kundi la kwanza la wanafunzi 18 katika programu ya elimu haina mwisho kurokea Zanzibar.
Amesema changamoto kubwa miongoni mwa jamii inayopelekea wanafunzi kukosa fursa ya kumaliza masomo ya sekondari ni pamoja na mimba, ufukara katika familia na kushindwa kuvumilia changamoto za kuoata elimu ikiwemo mwendo wa umbali mrefu kufika mashuleni miongoni mwa wanafunzi.
Aisha Haji mmoja wapo wa wanafunzi wanaosomea umeme katika chuo cha wananchi Kilwa Masoko ameishukuru serikali kwa fursa ya kurudi darasani na taasisi za Mwanamke Initiatives foundations na KTO kwa msaada wa vifaa na mahitaji muhimu.
Mkuu wa chuo cha wananchi cha Kilwa Masoko, Elabry Miyombe amesema amefurahi kupokea misaada kutoka kwa wadau hao.
Amesema miongoni mwa changamoto zinazowakabili wanafunzi hao ni kukosa mahitaji maalum ya kila siku na vifaa vya shule.